MOSHI-KILIMANJARO
Uongozi wa Bodi ya
Maji Bonde la Pangani, umesikitishwa na tabia ya baadhi ya wananchi ambao
wamegeuza maeneo ya vyanzo vya maji kuwa sehemu ya dampo la kutupa takataka, ambazo
wamekuwa wakizizalisha majumbani mwa.
Mkurugenzi wa Bodi ya Maji Bonde la Pangani (PBWB) Mhandisi Segule Segule, ameyasema hayo Oktoba 23, 2024, wakati akizungumza na waandishi wa habari, mara baada ya kutembelea na kukagua udabuaji wa tope lililokuwa limejaa kwenye wa mto Rau baada ya mafuriko yaliyotokea mwanzoni mwa mwaka huu na kuathiri familia nyingi katika kata za Mji Mpya na Msaranga zilizoko halmashauri ya Manispaa ya Moshi, Mkoani Kilimanjaro.
“Vyanzo vya maji kazi
yake kubwa ni kutupitishia maji ambayo tunayatumia kwenye matumizi mbalimbali, lakini
wako baadhi ya watu wameyageuza maeneo haya na kuwa ni maeneo ya kutupa
takataka wanazozizalisha majumbani mwao,”amesema Mhandisi Segule.
Aidha ameziomba Mamlaka zinazohusika kuhakikisha kwamba wanashirikiana kwa pamoja na Bonde la Pangani
katika kudhibiti tabia hiyo ya utupaji wa taka taka katika vyanzo vya maji.
“Sisi Bodi ya Maji Bonde la Pangania hatuwezi kufika kila eneo, kila mtu anatakiwa kutoa mchango wake katika kutunza vyanzo hivi vya maji, kama hatuta vitunza vyanzo hivi kuna hatari kubwa ya vyanzo vya hivi vya maji kukauka kutokana na uharibifu huu,”
Katika hatua nyingine Mkurugenzi huyo amewataka wananchi wanaoishi katibu na mto Rau, kuheshimu
mipaka ya vyanzo vya maji ili kupunguza athari za mafuriko kutokea na hivyo kulinda
mazingira.
Amesema kuwa wako wananchi,
wamejenga makazi na kufanya shughuli za kilimo ndani ya mita 60 kutoka vyanzo
vya maji, ambao wamekuwa chanzo kikubwa cha mafuriko yanayotokea pindi mvua za
vuli na masika zinapoanza kunyesha.
“Wananchi wanaofanya
shughuli karibu na nyanzo vya maji ikiwemo mito ndio wamekuwa chanzo kikubwa cha
uharibifu wa mazingira na hivyo kusababisha mafuriko kutokea pale mvua
zinapoanza kunyesha,”amesema Mhandisi Segule.
Ameongeza kuwa “Niwatake wananchi kuzingatia kanuni za kutofanya shughuli zao ndani ya mita 60 kutoka vyanzo vya maji vya mto huu kwani zinasababisha kingo za mito kubomoka na kusababisha mto kukosa muelekeo na kuleta mafuriko.”amesema.
Kwa upande wake Diwani Kata ya Mji Mpya Abuu Mohamed Shayo, ametoa wito kwa uongozi wa (PBWB) kuweka alama za mipaka (beacon)
zitakazoonyesha mipaka inayotenganisha makazi ya watu na eneo lililotengwa ili
kuepusha uvamizi.
"Kuna watu wanaodai kuwa maeneo ya karibu na mto Rau ni mali yao wakati dalili zote zinaonyesha eneo hilo limehifadhiwa; uamuzi wa kuweka alama hizo za mipaka utaondoa utata", amesema.










