Kikosi maalumu cha Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWT) kilichokuwa kimepandisha Mwenge wa Uhuru na Bendera ya Taifa katika kilele cha mlima Kilimanjaro.
MOSHI-KILIMANJARO
Waziri
wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa Dkt. Stergomena Tax, amekipongeza kikosi
maalumu cha Jeshi la Wananchi Tanzania (JWT) kwa kuonesha ukakamavu, uzalendo
na umahiri katika kufikisha Mwenge wa Uhuru pamoja na Bendera Taifa kwenye kilele
cha mlima Kilimanjaro.
Waziri
Tax ametoa pongezi hizo Oktoba 21, 2024, wakati wa kukipokea kikosi hicho kilichopandisha
Mwenge wa Uhuru na Bendera ya Taifa katika kilele cha mlima Kilimanjaro, hafla
iliyofanyika katika Geti la Marangu Wilaya ya Moshi mkoani Kilimanjro na kuhudhuriwa
na viongozi mbalimbali akiwemo Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro pamoja na Watendaji
wa Taasisi za Serikali.
Waziri
Dkt. Stergomena Tax amesema kuwa, kupandishwa kwa Mwenge wa Uhuru kwenye kilele
cha mlima Kilimanjaro ni ishara ya kusherehekea miaka 60 ya historia yetu na kutukumbusha
wajibu wa kulinda Uhuru kwa kujenga Taifa lenye Umoja, Mshikamano, na Maendeleo.
“Naomba
niwapongeze sana kwa kazi nzuri wanayoifanya Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWT)
kazi mnayoifanya ni kubwa, ambapo sote tuna Amani, Taifa letu liko Imara, tunao
mshikamano, mipaka yetu iko salama si kwa sababu iko salama tu…ni kwasababu ya
kazi kubwa inayofanywa na Jeshi letu hili,”amesema.
Akizungumza
katika hafla hiyo Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi Jenerali Jacob Mkunda, amesema,
ametekeleza agizo alilopewa kwa uangalifu mkubwa na Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi
ya Ulinzi na Usalama na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia
Suluhu Hassan.
“Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na
Usalama Dkt. Samia Suluhu Hassan, alinipatia Jeshi la Wananchi wa Tanzanaia,
jukumu la kupeleka Bendera ya Taifa na Mwenge wa Uhuru kupeleka katika kilele
cha mlima Kilimanjaro, mimi kama CDF
nilipokea jukumu hili kwa niaba ya Jeshi la Wananchi wa Tanzania,”amesema,
Ameongeza
kuwa “Jeshi la Wananchi wa Tanzania limetekeleza agizo la Amiri Jeshi Mkuu kwa
weledi, uaminifu na uangaligifu mkubwa.”amesema.
Aidha
Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi Jenerali Jacob Mkunda, ametoa shukrani kwa Hifadhi ya
Taifa Kilimanjaro kwa kutoa ushirikiano muhimu kwa timu nzima.
Oktoba
14, 2024, Rais Samia Suluhu Hassan alimkabidhi Mwenge na Bendera ya Taifa
Jenerali Mkunda ili Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWT) waweze kupandisha Mwenge
wa uhuru na Bendera ya Taifa katika kilele cha mlima Kilimanjaro, ambapo safari ya kuupandishi Mwenge wa Uhuru ilianza Oktoba
15 na kukamilika rasmi Oktoba 21, kwa furaha kubwa baada ya mafanikio ya
kurejesha Mwenge salama.






