MOSHI-KILIMANJARO.
Jumla ya watu 1,090,312
wamejiandikisha mkoani Kilimanjaro kwa ajili ya kushiriki uchaguzi wa Serilali
za Mitaa mkoani unaotarajiwa kufanyika Novemba 27, mwaka huu.
Hayo yameelezwa Oktoba 21,2024
na Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro Nurdin Babu, wakati akitoa taarifa inayohusiana
na zoezi hilo, ambapo amesema idadi hiyo ni asilimia ya lengo lililowekwa la
kuandikisha watu 1,172,394.
“Kati ya waliojiandikisha ni
wanaume walikuwa 544,189 na wanawake ni 546,123 na kwamba wilaya ya Mwanga
ndiyo iliyoongoza kimkoa, kwa kuvuka malengo yaliyowekwa ya uandikishwaji
wilayani humo”, amesema.
Ameongoze, “Halmashauri ya
wilaya Mwanga iliandikisha jumla ya watu 92,112 sawa na asilimia 100.9 ya lengo
lililokuwa limewekwa la kuandikisha watu 91,327”.
Kwa mujibu wa Babu, halmashauri
za wilaya zingine ni pamoja na Same iliyoandikisha watu 180,649 sawa na
asilimia 100.0 ya lengo la kuandikisha watu 180,587.
Babu amezielezea takwimu za
uandikishwaji za halmashauri za wilaya zingine na malengo yake kwenye mabano
kuwa ni Siha 79,749 (81,501), Moshi Manispaa 144,213 (149,937) na Rombo 155,601
(171,330).
Aidha amezitaja halmashauri
zingine kuwa ni Halmashauri ya wilaya ya Moshi (Moshi-DC) 306,178 (344,715) na
kwamba halmashauri ya wilaya ya Hai imeandikisha jumla ya watu 131,810 ikilinganishwa
na malengo ya kuandikisha watu 152,997.
Katika hatua nyingine Babu ametoa shukrani kwa watu waliojitokeza katika kushiriki zoezi la uandikishwaji kwa ajili ya kujiandaa kwa uchaguzi utakaofanyika baadaye mwaka huu.
“Nitoe wito kwa wananchi
kujitokeza kwa wingi huo wakati wa kuchukua fomu na hata kampeni zitakapoanza.”amesema
Babu.
Amesema “Uchaguzi huu una
faida kubwa kwa wananchi kutokana na ukweli kuwa viongozi watakaochaguliwa
ndiyo wenye dhamana ya kushughulikia shughuli za kimaendeleo kwenye maeneo
wanayotoka”, amesema.
Ameongeza, “Viongozi wa
ngazi za mitaa ndiyo waliokaribu zaidi na wananchi, hivyo wao ndiyo wa kwanza
kujua mahitaji ya wananchi ya kimaendeleo; wakishabaini mahitaji husika ndiyo
serikali kuu nayo inakuja na mipango ya kuleta maendeleo hayo”.
Wakizungumzia mchakato huo
wa uandikishaji wa wapiga kura kwenye daftari la wapiga kura Mwenyekiti wa Chama
cha Sauti ya Umma (SAU) mkoani Kilimanjaro Isaack Kireti na Mwenyekiti wa Chama
cha Wananchi (CUF) Wilaya ya Moshi Habibu Hamisi Msangi, wamesema kuwa zoezi
hilo limekwenda vizuri.
“Kikubwa tulichokibaini
hapa ni uhamasishaji mkubwa uliofanywa na mamlaka husika kwa wananchi wajitokeza
kujiandikisha; haijawahi kutokea uhamasishaji wa aina hii kwa miaka mingi
iliyopita”, wamesema.
Aidha viongozi hao wametoa wito kwa wananchi kujitokeza kwa wingi kugombea nafasi zilizoko ili wapatikane viongozi ambao wako karibu na wananchi na ambao watakuwa tayari wa mbele kuwahudumia wananchi.
