MOSHI-KILIMANJARO.
Halmashauri ya Wilaya
ya Mwanga mkoa wa Kilimanjaro, imevunja rekodi ya uandikishaji wa orodha ya
Wapiga Kura, Uchaguzi wa Serikali za Mitaa na hivyo kusika nafasi ya kwanza kimkoa.
Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro
Nurdin Babu, ameyasema hayo Oktoba 21,2024 wakati akitoa taarifa inayohusiana
na zoezi hilo kwa waandishi wa habari ofisini kwake, ambapo amesema halmashauri
ya Wilaya Mwanga iliandikisha jumla ya watu 92,112 sawa na asilimia 100.9 ya
lengo lililokuwa limewekwa la kuandikisha watu 91,327.
Kwa mujibu wa Babu, amesema
halmashauri iliyoshika nafasi ya pili ni Same iliyoandikisha watu 180,649 sawa
na asilimia 100.0 ya lengo la kuandikisha watu 180,587.
Amesema nafasi ya tatu
imeshikwa na halmashauri ya Wilaya ya Siha iliyoandikisha watu 79,749 sawa na
asilimia 97.9 huku nafasi ya nne ikishikwa na Halmashauri ya Manispaa ya Moshi
ambayo iliandikisha watu 144,213 sawa na asilimia 96.2 ambapo makadirio ilikuwa
ni kuandikisha watu (149,937).
Babu alizielezea takwimu uandikishwaji
za halmashauri za Wilaya zingine na malengo yake kwenye mabano kuwa ni Rombo watu
155,601 sawa na asilimia 90.8, ambapo malengo ilikuwa ni kuandikisha watu 171,330.
Aidha amezitaja halmashauri zingine kuwa ni Halmashauri ya Wilaya ya Moshi (Moshi-DC) watu 306,178 sawa na asilimia 88.8 (344,715) na kwamba halmashauri ya Wilaya ya Hai imeandikisha jumla ya watu 131,810 sawa na asilimia 86.2, ikilinganishwa na malengo ya kuandikisha watu 152,997.
