MOSHI-KILIMANJARO
Mkuu wa Wilaya ya Moshi James Kaji, amewataka Vijana kuachana na
matumizi ya dawa za kulevya na badala yake waungane katika kufanya shughuli
halali za kiuchumi ili wajiletee maendeleo katika ngazi ya familia, jamii na
hata Taifa.
Kauli hiyo jana, wakati akizungumza kwenye Tamasha la ‘Vijana na Uongozi
Festival’ lililofanyika kwenye viwanja vya Polisi Himo na kuhudhuriwa na vijana
takribani 200 kutoka kata 32 za Wilaya hiyo.
Kaji amesema kwa sasa kuna wimbi kwa baadhi ya vijana kutumika kusafirisha bange,
mirungi na kuwaonya kujiepusha kabisa na usafirishaji wa dawa za kulevya kwani
wakikamatwa wataishia gerezani.
“Kwa Wilaya yetu ya Moshi tatizo hili
la vijana kutumika kusafirisha mirungi,
bangi na wahamiaji haramu ni kubwa, watu wasilifumbie macho, kwa taarifa za
polisi kila kila siku, wanaokamatwa na usafirishaji
wa dawa za kulevya aina ya mirungi na bangi vi vijana,”amesema.
Amesema wako pia baadhi ya
vijana wanatumika kusafirisha wahamiaji haramu kuwavusha mpakani na
kuwahifadhi, ulevi wa gongo kupindukia, tatizo hili ni kubwa sana katika wilaya
ya Moshi.
Aidha mkuu huyo wa wilaya ametoa
rai vijana ambao hamjaingia kwenye usafirishaji wa dawa hizo, lakini pia na
utumiaji wa pombe aina ya gongo, wasishawishike kuingia huko na wale ambao wameshaathirika na dawa amewataka
kuendelea kutumia dawa za kuwakinga ili wasiathirike zaidi.
Katika hatua nyingine Kaji, alitumia fursa ya tamasha hilo kuwataka vijana
kuwa na maadili mema pomoja na kujiepusha na makundi ya ushawishi ili kulinda
afya zao na nguvu kazi ya taifa.
“Nitumia tamasha hili kuwataka vijana mjikite zaidi na Shughuli za
kimaendeleo, ikiwemo ufugaji, kilimo na ujasiriamali, lakini pia nendeni mabalozi
wazuri kwa kuwaelimisha wale wote ambao hawakupata
nafasi ya kushiriki katika tamasha hili, kuhusu athari na madhara ya matumizi
ya dawa za kulevya kwa ustawi wa jamii na Taifa kwa ujumla.”amesema.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa UVCCM Wilaya ya Moshi vijijini Yuvenari Shirima,
alisema kupitia tamasha hilo pia vijana watapatiwa elimu ya fedha ili
kuwajengea uwezo wa kufanya maamuzi sahihi ya kupata na kutumia huduma za fedha
hapa nchini.
“Elimu ya Fedha ni program inayotolewa kwa kuzingatia mwongozo wa
mkakati wa maendeleo ya Sekta ya Fedha, ziko taasisi mbali za kifedha
zitakwenda kuwapatia elimu juu ya masuala elimu ya fedha na mwongozo huo ambao
pamoja na mambo mengine ni lazima vijana hawa wapate elimu ya fedha katika
makundi mbalimbali kama vile Vyama vya Ushirika, Wanafunzi, Waalimu,
Wafanyakazi, Vikundi vya huduma ndogo za fedha na Wananchi kwa ujumla.”amesema.
Ameongeza kuwa Rais Samia ameruhusu kuanza kutolewa kwa mikopo isiyokuwa
na riba kwa wanawake, vijana na watu wenye ulemavu na kwa halmashauri ya halmashauri
ya Moshi kuna zaidi ya milioni 800.
Naye Katibu wa UVCCM Wilayani humo Malkiori Pantaleo, amekiri kuweko kwa
baadhi ya vijana kujiingiza kwenye unywaji wa pombe aina ya gongo kupindukia.



