Miongoni mwa nyumba iliyobomolewa kupisha mradi wa ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami.
SAME-KILIMANJARO
WANANCHI wa
tarafa za Gonja, Ndungu na Bendera, Wilaya ya Same Mkoani Kilimanjaro, wamemuomba
Rais Samia Suluhu Hassan, kuingilia kati swala la wao kutokulipwa fidia baada
ya kutakiwa kuvunja nyumba zao ili kupisha ujenzi wa barabara kwa kiwango cha
lami.
Wakiongea na Waandishi wa
habari kuhusiana na swala hilo, wananchi hao wamesema kuwa swala hilo
limewasababishia usumbufu mkubwa na kwamba Rais tu ndiye anayeweza kuwasikiliza
ili wapate haki zao.
Mkazi wa Kata Ndungu Mlavi
Mohamed, amesema kuwa waliarifiwa kuwa kuna mradi huo wa barabara ambao utaenda
sambamba na upanuzi wa barabara hiyo ya Same-Kisiwani-Mkomazi.
“Mara ya kwanza walikuja
wakapima, wakaja wakatufanyia tathmini wakatupiga picha, wakatuambia watatulipa,
baada ya hapo wakaja tena kwa mara ya pili wakatuambia hatutalipwa na wakatupa muda
wa siku 30 wakitutaka tuvunje nyumba zetu,”amesema Mohamed.
Ameongeza kuwa “Hali hii
imeniathiri sana kiuchumi, nimebomoa nyumba zangu saba ambazo zote zilikuwa na
wapangaji, ambao walikuwa wamelipa kodi
zao,”amesema.
Akisimulia zaidi Mohamed, amesema
kuwa mara ya kwanza walikuja wapimaji wakapima nyumba zilizokuwa eneo la
barabara zikawekewa alama za kuonyesha kuwa ziondolewe ambapo waliambiwa
watalipwa fidia.
“Mara ya pili wakaja
wapimaji wengine ambao walipima na kuongeza idadi ya nyumba ambazo hazikuwekewa
lama ya kuondolewa mara ya kwanza na hizi tumeambiwa wahusika wake hawatalipwa
fidia”, amesema.
“Tumepewa mwezi mmoja
kuziondoa nyumba zetu wenyewe na baada ya hap wale ambao hawakuwa wameziondoa
nyumba zao zitaondolewa na kisha wenye nyumba hizo tumeambiwa tutatakiwa kuwalipa
fidia wale watakaokuja kuzivunja”, amesema.
Mkazi huyo alihoji ni
kwanini upimaji umefanyika mara mbili na ile ya pili hawatalipwa fidia na tena
waziondoe wenyewe huku wakitishiwa kuwa zitavunjwa na mamlaka husika halafu
tuwalipe kazi hiyo kuvunja nyumba zetu.
“Tunachojiuliza hapa ni je,
wale waliopima kwanza si wa serikali? Na kama ni wa serikali ni je hawajui kazi
zao kiasi cha kwamba wananchi tunapata usumbufu usio na sababu?”, alihoji mkazi
huyo.
Mkazi wa Ndungu Sufiani
Mvule, amesema suala la ujenzi wa barabara katika Jimbo la Same Mashariki,
limekuwa ni suala la wana siasa kujitafutia mtaji wao wa kupata kura.
“Bomoa bomoa inayoendelea
imetuathiri kwa kiasi kikubwa sana, kwanza namna notisi iliyotolewa ni ya muda
wa mwezi mmoja, wako baadhi ya watu kwa sasa wamehifadhiwa na ndugu zao kwa
kuwa hawana tena hela za kujenga.”amesema.
Wakazi wengine wa kata ya
Bendera Zakia Richard na Rabia Haji, wamesema kuwa wanapenda kuwa na maendeleo,
ila kilio chao kifikiriwe maana wao kama Watanzania wengine wana haki ya kuwa
na makazi mazuri hata kama watatoa maeneo yao kwa ajili ya maendeleo.
“Ni kweli mradi huu wa
barabara ni swala la kimaendeleo na hata shughuli za kibiashara zitakuwa, ila
tunachoomba mamlaka husika iweze kutulipa fidia ili tuweze kujenga nyumba
nyingine za kuishi”, wamesema.
Mwananchi mwingine Asha Bakari
Kibwana mkazi wa Ndungu, amekiri kupokea notisi ya mwezi mmoja inayomtaka
avunje nyumba yake ndani ya siku 30 ili kupisha ujenzi wa barabara hiyo.
Amesema alifiwa na mwanae mwezi Julai 27 na kumzika Julai 29 mwaka huu
na ilipofika mwezi Agosti 6 mwaka huu aliletewa notisi ya kutakiwa kubomoa
nyumba yake ili kupisha ujenzi wa barabara.
“Mimi maendeleo sikatai,
ila tunachokiomba serikali iweze kutupa fidia ili tuweze kwenda kununua maeneo
mengine tuweze kujenga, lakini cha kushangaza wametuletea notisi ya kututaka
tubomoe nyumba na fidia wamesema hatutalipwa,”alisema.
Alipotakiwa kuzungumzia
swala hilo Meneja wa Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads) mkoani Kilimanjaro
Mhandisi Motta Kyando amesema hayuko tayari kuzungumzia swala hilo kwa sasa
kutokana na kuwa swala hilo liko ngazi ya juu kiofisi.
Aidha Kyando, amesema
ujenzi wa barabara hiyo ukikamilika utafungua uchumi wa wakazi wa Wilaya ya
Same, ambao kwa kiasi kikubwa wanategemea shughuli za kilimo cha mazao ya tangawizi,
mpunga na ndizi na kuhuisha utalii
katika Hifadhi ya Taifa ya Mkoamazi.
“Barabara ya Same-Kisiwani –Mkomazi
ina urefu wa kilometa 98 inatarajiwa kugharimu kiasi cha Sh bilioni 68 na
kwamba kukamilika kwake itatoa fursa za kiuchumi na utalii kwa wananchi wa
ukanda wa milimani ambao wengi ni wakulima wa mazao mbalimbali ikiwemo
Tanzngawzi, mpunga na mazao mengine.
Kuhusu barabara ya Ndungu-Mkomazi,
Mhandisi Kyando alisena ina kipande cha kilometa 36.9, ambapo tayari serikali
kupitia Wakala wa Barabara imesaini mkataba wa kuweza kuanza kazi ya ujenzi kwa
kiwango cha lami.
“Mkataba huu ulisainiwa
mwezi Januari mwaka huu, ambapo mradi huo utachukua miezi 18 na kwamba ifikapo mwezi
Desemba mwaka 2025 kazi ya ujenzi itakuwa imekamilika.”amesema.
Mhandisi Kyando ameongeza
kusema kwamba barabara hiyo endapo itakamilika itakuwa na manufaa makubwa sana,
kwani kutakuwa na maendeleo makubwa kwa,
vijana ambao watapata ajira na
kukuza uchumi baada ya watalii
kuongezeka na watu wataona urahisi wa kufika katika hifadhi ya mkomazi.

