Waziri Ridhiwani Kikwete amesema Tanzania inaendelea kutimiza maono ya Hayati Mwalimu Julius Nyerere chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan.
Kikwete amesema hayo mnamo Oktoba 15,2024 katika Hifadhi ya Taifa ya Mlima Kilimanjaro wakati wa hafla ya kupokea kikosi maalumu cha Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) ambacho kimepewa jukumu na Rais Samia Suluhu Hassan la kupeleka Mwenge wa Uhuru na Bendera ya Taifa ya Tanzania kilele cha mlima Kilimanjaro.
“Tanzania inapeleka Mwenge wa Jhuru juu ya Mlima Kilimanjaro ili kuitangazia Dunia kuwa Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ni imara na pia utaendelea kulinda Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar.”amesema Kikwete.
Waziri Kikwete amesema kuwa kwa mwaka huu 2024, Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ameamuru Mwenge wa Uhuru upelekwe juu ya Mlima Kilimanjaro baada ya kuhitimisha mbio zake kwa siku 195.
Akizungumzia uharibifu wa mazingira na changamoto za mabadiliko ya tabia nchi Waziri Kikwete, amesema kwamba ni muhimu kwa Watanzania kuendelea kuhifadhi mazingira ili kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi.
“Kutokana na changamoto hizi, hatua za ziada zinahitajika ili kulinda rasilimali za asili pamoja na ustawi wa viumbe hai na kuifanya dunia kuendelea kuwa sehemu ya kuishi.”amesema.
Aidha amesema kuwa upelekwaji wa Mwenge wa Uhuru katika kilele cha mlima Kilimanjaro, unalenga kutangaza utalii wa Tanzania, akitaja filamu ya Royal Tour kama mfano wa juhudi za kuendelea kuutangaza utalii.
Awali Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi, Dkt. Pindi Chana amesema kupandishwa Mwenge wa Uhuru Mlima Kilimanjaro mwaka huu 2024 kunaleta hamasa ya uzalendo kwa wananchi hususan wakati huu ambao Tanzania inaadhimisha miaka 60 ya Uhuru na mafanikio ya Taifa.
“Tunampongeza Rais Samia kwa wazo lake la kuupandisha Mwenge wa Uhuru Mlima Kilimanjaro ambapo utachangia kuutangaza utalii wa Tanzania.”amesema.
Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Nurdin Babu amemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuridhia Mwenge wa Uhuru, kupandishwa kwa mara nyingine katika kilele cha Mlima Kilimanjaro.
Akizungumza kiongozi wa kikosi maalumu cha makamanda wa Jeshi la Wananchi Tanzania JWT Luten Kanali Khalid Hamis Hamad, amehaidi kuwa watatekeleza jukumu walilopewa la kufikisha Mwenge wa Uhuru pamoja na Bendera ya Taifa katika kilele cha mlima Kilimanjaro na kuwaomba Watanzania wote kuwaombea.
Mwenge Uhuru uliwashwa mkoani
Kilimanjaro Aprili 2, 2024 na umekimbizwa kwa siku 195, ambapo jumla ya wanajeshi
21, ambapo Oktoba 15,2024 kikosi hicho kilianza safari ya kuelekea katika
kilele cha mlima mrefu Barani Afrika mlima Kilimanjaro.





