Makada wa CCM Moshi Mjini waanza kuchafuana kwa fitina za kisiasa


Mlezi wa CCM Mkoa wa Kilimanjaro ambaye pia ni Katibu wa NEC Siasa na Uhusiano wa Kimataifa Rabia Abdallah Hamid, Akizungumza na Kamati ya Siasa ya Mkoa, Sektarieti pamoja na Wajumbe wa Halmashauri Kuu za CCM za Wilaya.

MOSHI-KILIMANJARO

Makada wawili wa Chama cha Mapinduzi CCM Moshi Mjini, mkoani Kilimanjaro wameanza kuchafuana kwa fitina za kisiasa.

Hayo yamejiri leo Oktoba 16, 2024 baada ya vipeperushi ambavyo vilikuwa vimezalishwa na kusambazwa mji mzima wa Moshi huku vingine vikiwa vimemwagwa kwenye Ofisi za Makao makuu ya CCM Mkoani humo.

Vipeperushi hivyo vimeandikwa, “Chama chetu ni kisafi, kisibebe watu wachafu,  mzee wa tindikali tajiri wa sheli….Mwenezi wa Manispaa ndio chanzo cha migogoro aondolewe chama kipoe.”

Kwa mujibu wa vyanzo vyetu vya ndani vinadai kuwa, makada hao wawili wa chama hicho kikuu cha siasa nchini, wanaotoka Moshi Mjini ambao wanaonekana kuwania nafasi ya ubunge wa Jimbo la Moshi Mjini 2025-2030.

Akizungumza na Kamati ya Siasa ya Mkoa, Mlezi wa Chama hicho ambaye pia ni Katibu wa NEC Siasa na Uhusiano wa Kimataifa Rabia Abdallah Hamid, amesema Moshi Mjini imekuwa kitovu cha fitina ndani ya Chama, hatua ambayo imekuwa ikiwapa upinzani nguvu ya kukikosoa hata Kama kinafanya vizuri.

Kikao hicho pia kimehudhuriwa na Sekretarieti ya mkoa, pamoja na Wajumbe wa Halmashauri za CCM za Wilaya saba za mkoa huo, ambapo mkutano wa uliofanyika Ukimbi wa CCM mkoani humo.

Aidha Mlezi huyo wa CCM Mkoa wa Kilimanjaro, amewataka kupunguza fitina za kisiasa kwa Ustawi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Maendeleo ya Watanzania kwa ujumla.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa CCM, mkoa wa Kilimanjaro Patrick Boisafi amesema siri ya mafanikio ipo katika umoja miongoni mwa wanachama wenyewe.

Naye Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Wilaya ya Moshi Mjini ambaye pia ni Mstahiki Meya wa Halmashauri ya Manispaa ya Moshi, Injinia Zuberi Abdallah Kidumo amekubali maneno ya Mlezi huyo na kuwataka wanasiasa wenzake kuzingatia wito uliotolewa. 

Katibu wa NEC Siasa na Uhusiano wa Kimataifa Rabia, amekuja mkoani Kilimanjaro wakati ambao zoezi la Uandikishaji wa orodha ya Wapiga Kura likiendelea ambalo linatarajiwa kumalizika mnamo Oktoba 20, 2024; kwa ajili ya Uchaguzi wa Serikali Mitaa utakaofanyika Novemba 27, mwaka huu.










Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.