MWANGA-KILIMANJARO
WANANCHI Mwanga, Mkoa wa Kilimanjaro, wameelezea shukrani zao kwa Serikali kwa kujenga hospitali mpya ya Wilaya, Ukanda wa Tambarare, ambayo imerahisisha upatikanaji wa matibabu na kupunguza safari za kutembea umbali wa kilometa 25 kwenda hospitali ya Wilaya Usangi iliyoko milimani kwa ajili ya kutafuta matibabu.
Cesilia amesema baadhi yao, walilazimika kutumia miti shamba na njia nyingine za asili kwa ajili ya kujitibu kutokana na umbali wa hospitali ya wilaya iliyokuwa imejengwa milimani.
“Sisi Wanawake wa Mwanga, tunaishukuru sana Serikali kwa kutujengea hospitali hii kwenye Ukanda wetu waTtambarare, kabla ya hapo mgonjwa anapougua alikuwa analazikika kupelekwa Usangi iliko hospitali ya Wilaya na sio wote walikuwa na uwezo wa kwenda huko, baadhi ya wananchi walitafuta njia mbadala za kujitibu, wengine walitumia miti shamba, ili kuweza kujitibu kutokana na gharama.”amesema Cesilia.
Mkazi mwingine wa Mwanga Hinja Solomoni Msuya, ameongeza kuwa Serikali imejibu changamoto za wananchi, akielezea hali ngumu ambayo wagonjwa walikumbana nayo, ambapo wengi walilazimika kusafirishwa kutoka Kata ya Toroha na Kwakoa hadi Usangi, umbali wa kilomita 25 iliko hospitali ya Wilaya.
Hinja ameyataja madhara makubwa yaliyokuwa yakiwakumba wananchi hao, akisema wengi walipoteza maisha kabla ya kufikishwa hospitali ya rufaa ya mkoa ya Mawenzi au KCMC.
Mkazi wa kitongiji cha Mikuyuni Juma Kiteri Amiri; ameishukuru Serikali kwa kuwajengea hospitali mpya ya wilaya ambayo itasaidia kuboresha huduma za afya katika eneo hilo na kupunguza matatizo yanayohusiana na ufikishaji wa wagonjwa.
“Usafiri ulikuwa ni changamoto, unapokuwa na mgonjwa inakubidi utafute gari la kukodi ilikuwa ni changamoto kubwa sana, kutokana na changamoto hiyo ilitulazimu kutumia miti shamba, tulikuwa tukichimba mizizi ya mijohoro na majani ya mwarobaini, tunaichemsha tunakunywa maji yake.”amesema Amiri.
Naye Mkazi wa mji mdogo wa Mwanga Joshua Mohamed; amesema “Tunafurahi sana kujengwa kwa hospitali eneo hili, mtu anapopata changamoto ya kuugua anaweza kuletwa katika hospitali ya wilaya ambayo iko tambarare na kuweza kutibiwa.”amesema.
Kwa upande wake Mganga mkuu wa Halmashauri ya Mwanga Dkt. Serijo Kusekwa, amesema mradi wa ujenzi wa hospitalli hiyo umetumia kiasi cha Sh bilioni 2.1 ikiwemo ununuzi wa vifaa vya ujenzi, malipo ya mafundi pamoja na ununuzi wa vifaa tiba vyenye thamani ya Sh milioni 449.
Aidha amesema kuwa hospitali hiyo tayari imeanza kutoa huduma za afya Mei mwaka huu ambapo jumla ya wananchi 1,093 wakiwemo akima mama wajawazito 235, watoto 587 na wananchi 271 wamepata huduma za afya.




