MOSHI-MANISPAA
Mstahiki Meya wa
Halmashauri ya Manispaa ya Moshi Mhandisi Zuberi Abdallah Kidumo, amewaongoza Wakazi wa Kata ya Njoro, kujiandikisha
katika Daftari la mpiga Kura kwa ajili ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa, huku
akiwataka kuendelea kujitokeza kushiriki zoezi hilo ili kujihakikishia haki yao
kikatiba ya kushiriki katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa na Uchaguzi Mkuu
mwaka 2025.
Zoezi la kujiandikisha
katika Daftari la Mpiga kura lilianza Oktoba 11, 2024 kwa nchi nzina na
linatarajiwa kufika ukomo wake Oktoba 20, mwaka huu.
Akiwa kwenye Kituo cha
mpiga kura Njoro mtaa wa Dobi Mstahiki Meya Kidumo, amekuwa ni miongoni mwa wakazi
wa kata hiyo, waliojiandikisha na baadae akawaasa wakazi wa kata hiyo
kulichukulia jambo hilo kwa umakini mkubwa.
“Niwaombe sana wakazi
wa Manispaa ya Moshi kwa ujumla, kujitokeza kwa siku hizi zilizopangwa na (TAMISEMI)
ili kuweza kujiandikisha kutoka Oktoba 11, mpaka Oktoba 20, 2024 ambapo
mkishajiandikisha katika Daftari la Mkazi, maana yake ndio mtakuwa mmepata
tiketi halali ya kuweza kuwa wapiga kura halali mwezi Novemba 27, 2024 .”amesema
Mhandisi Kidumo.
Mstahiki Meya huyo
amesema kuwa Wananchi wanaostahili kushiriki uchaguzi huo ni Watanzania wenye
umri wa kuanzia miaka 18 na kuendelea, wenye akili timamu na ambao hawatumikii
kifungo gerezani.
Amesema viongozi
watakaochaguliwa katika uchaguzi huo ni Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji na
Wajumbe wa Halmashauri ya Kijiji ambao jumla yao watakuwa si chini ya 15 na
hawatazidi 25.
Katika ngazi ya mtaa, Kidumo
amesema Wakazi wa mtaa husika watamchagua Mwenyekiti na Wajumbe wa Kamati ya
mtaa, jumla ya viongozi wote watakuwa
watatu, na hawatazidi watano.
Aidha amesema katika
ngazi za vitongoji wakazi wote wa kijiji
husika wenye sifa ya kupiga kura
watawachagua Wenyeviti wa vitongoji vyote vya kijiji hicho ambao
kiutawala watakuwa sehemu ya uongozi wa kijiji husika.
Pia amesisitiza kwamba
yeyote ambaye hatajiandikisha katika Daftari la Wakazi hatakuwa na haki ya
kuwachagua viongozi wala kuchaguliwa kuwa viongozi katika ngazi husika.
Ameongeza kuwa
masharti kwa wenye nia ya kugombea nafasi yoyote ya uongozi katika uchaguzi huo
ni raia wa Tanzania, wakazi wa eneo husika, walioteuliwa na chama cha siasa
chenye usajili wa kudumu.
Vilevile amesema kuwa wagombewa
watatakiwa kuwa wanaojua kusoma na kuandika kwa lugha ya kiswahili au kiingereza,
wenye umri usiopungua miaka 21, wenye akili timamu na ambao hawatumikii kifungo
gerezani.




