
Mwenyekiti wa (UVCCM ) Wilaya ya Moshi Vijijini Yuvenari Shirima, akizungumza kwenye Tamasha la Vijana na uongozi , lililofanyika katika viwanja vya polisi himo katika Kata ya Makuyuni kwa lengo la kuwahamasisha vijana kujitokeza kugombea nafasi mbalimbali za uongozi Serikali za Mitaa 2024
MOSHI-KILIMANJARO
Umoja wa
Vijana wa Chama cha Mapinduzi (UVCCM) Wilaya ya Moshi Vijijini, umewataka Vijana Wilayani humo, kujitokeza kwa wingi kugombea
nafasi mbalimbali za uongozi katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa utakaofanyika
Novemba 27 mwaka huu.
Mwenyekiti wa
(UVCCM) Moshi Vijijini Yuvenari Shirima, ametoa
wito huo Oktoba 19, 2024 wakati
akizungumza kwenye Tamasha la ‘Vijana na
Uongozi Festival’ lililofanyika kwenye viwanja vya Polisi mji mdogo wa Himo
na kuhudhuriwa na vijana takribani 200 kutoka kata 32 za Wilaya hiyo.
Shirima
amewashauri vijana kuacha kulalamika kwamba hawapewi nafasi za uongozi na
kuwataka wajitokeze kuchukua fomu za
kugombea nafasi mbalimbali ili wapate nafasi za kuongoza nchi yao kwa vyeo
mbalimbali ikiwemo ya Uenyekiti wa Serikali za Vijiji, Vitongoji na Mitaa kwani
nao wana mawazo chanya.
Aidha amesema
Chama cha Mapinduzi (CCM) kinawapa fursa vijana wote kugombea nafasi mbalimbali
za uongozi kwani Tanzania ya leo na kesho inaundwa na kundi la vijana.
“Serikali
iliyopo madarakani chini ya usimamizi wa Rais Samia Suluhu Hassan, imekuwa
ikiwatengeneza vijana kuanzia kwenye elimu, kwani inawapa mikopo ya elimu ya
juu wasome, lakini pia imetenga fedha kila halmashauri kwa ajili ya mikopo
isiyo na riba ili wajikwamua kiuchumi,” amesema Shirima.
Awali
akizungumza Katibu wa UVCCM Wilaya ya Moshi Vijijini Malkiori Pantaleo, amesema
tamasha hilo ni mwendelezo wa matamasha ambayo wamekuwa wakiyafanya ili kuwahamasisha vijana kujitokeza kugombea nafasi mbalimbali za uongozi kwenye Uchaguzi wa
Serikali za Mitaa.
“Lengo la tamasha hili ni kuwahamasisha
vijana kujitokeza kugombea nafasi mbalimbali za uongozi na huu ni mwendelezo wa
matamasha ambayo tumeshayafanya katika kata za Mwika Kusini, Kibosho na Mwika Kaskazini,”amesema
Pantaleo.
Naye Katibu
wa UWT Moshi Vijijini Olva Ngalawa, amewahamasisha Wanawake Wilayani humo,
kuunga mkono juhudi za Rais Samia Suluhu Hassan za matumizi ya Nishafi safi ya
kupikia katika maeneo mbalimbali ili kusaidia kutunza mazingira, kuokoa muda,
kuimarisha afya na Uchumi.
Kwa upande
wake Mkuu wa Wilaya ya Moshi James Kaji, amesema ili waweze kumchagua kiongozi
bora atakayewaletea maendeleo katika vijiji na vitongoji vyao vijana hawana
budi, kujitokeza kushiriki kugombea nafasi hizo za uongozi.
Tamasha hilo,
lilikuwa limebeba Kauli Mbiu ‘Wakati Wetu Ndo Sasa Vijana Tujitokeze Kugombea”
ni mwendelezo wa matamasha ambayo UVCCM imekuwa ikiyafanya kwa lengo la kuwahamasisha
vijana kushiri Uchaguzi wa Serikali za Mitaa na Uchaguzi Mkuu mwaka 2024.














