SIHA-KILIMANJARO
Wilaya ya Siha, imepokea
mtambo wa kuchimba visima virefu vya maji, ambapo mtambo huo utakwenda kuchimba
visima vya maji katika maeneo kadhaa ya Wilaya hiyo ambayo hayana vyanzo vya
maji ya mserereko (mtiririko).
Meneja wa Wakala wa Maji na
Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) Wilaya ya Siha Injinia Emmy George,
amesema hayo Oktoba 14, 2024 ofisini kwake, wakati akizungumza na Waandishi wa
habari wilayani humo.
Amesema mtambo huo
utakwenda kuchimba visima vitano vya maji vitakavyosaidia kuboresha huduma ya
maji katika wilaya hiyo na kuondoa changamoto ya maji katika baadhi ya vijiji vilivyoko katika wilaya hiyo.
“Ruwasa tuna mpango wa kuanza
kuchimba visima vitano katika wilaya yetu ya siha, ambapo tayari tumeshaainisha
maeneo ambapo visima hivyo vitachimbwa, kisima cha kwanza kitachimbwa hospitali
yetu ya wilaya, kisima cha pili kitachimbwa kati ya kijiji cha Miti miteru au
Karimaji, kisima cha tatu Kandashi,”amesema.
Injinia Emmy ameongeza kuwa visima hivyo
vitakapo kamilika vitakwenda kuongeza upatikanaji wa maji kwenye mfumo wa maji
uliopo kwa sasa.
Aidha amesema kuwa tayari wataalamu
kutoka Bodi ya maji Bonde la Pangani (PBWB)
walikwishapita katika maeneo hayo kupima na kubainisha maeneo yanayoweza
kuchimbwa na kupatikana maji hayo na
kwamba utekelezaji wa kazi hiyo unakwenda kuanza mara moja ikiwa ni jitihada za
kumtua mama ndoo kichwani.
“Mitambo hii inakwenda
kuanza kazi katika maeneo ambayo hayana vyanzo vya maji vya mserereko.”amesema Injinia Emmy.
Pia meneja huyo wa Ruwasa wilaya
ya Siha, amesema kuwa kwa mwaka 2024 Ruwasa imefanikiwa kukamilisha mradi mmoja
wa maji unaohudumia kata ya Ngarenairobi.
“Tumeshakamilisha mradi mmoja
wa maji ambao unahudumia Bodi ya Maji ya Lawate- Fuka, ambao tumeutoa kwenye
chanzo kipya cha maji mto Sakana, takribani umbali wa kilometa 13 yalipo
matenki ya maji.”
Amesema kupitia mradi huo,
wananchi wa maeneo ya Sinai ambao walikuwa na changamoto kubwa ya maji kwa sasa
wanapata huduma ya maji safi na salama.
Serikali kupitia Wizara ya
Maji imeweka mkazo katika kuhakikisha kwamba wananchi wanapata huduma ya maji
safi na salama kwa karibu na maeneo yao.