Mkuu
wa Wilaya ya Moshi James Kaji, akikata utepe kuashiria ufunguzi wa Kahawa Festival-2024,
msimu wa Tano, Septemba 4,2024 hafla iliyofanyika katika Kiwanda cha kukoboa
Kahawa cha Tanganyika Coffee Curing kilichopo mjini Moshi mkoani humo.
MOSHI-KILIMANJARO
Wadau wa Kahawa Mkoani
Kilimanjaro wametakiwa kuanzisha mashindano ya Kahawa Marathon ili kuongeza unywaji
wa kahawa ya ndani kutoka asilimia 7 hadi kufikia asilimia 15 ifikapo mwaka
2025.
Mkuu wa Wilaya ya Moshi James
Kaji, ameyasema hayo mnamo Septemba 4,2024 wakati wa ufunguzi wa Tamasha la Tano la Kahawa “Kahawa Festival-2024,” ufunguzi uliofanyika katika kiwanda cha
kukoboa Kahawa cha Tanganyika Coffee Curing kilichopo mjini Moshi mkoani humo.
Amesema kuanzishwa shindano hilo
la Kahawa Marathon litakuwa ni hatua muhimu katika kuimarisha utamaduni wa
kahawa nchini na kutoa fursa za kiuchumi kwa wazalishaji wa kahawa.
Amesema uanzishwaji wa
mashindano hayo ya ‘Kahawa Marathon’ yataleta mabadiliko makubwa katika unywaji
wa kahawa ya ndani na hivyo kuongeza kiwango cha unywaji wa kahawa kutoka
asilimia 7 ya sasa hadi kufikia asilimia 15 ifikapo mwaka 2025.
Amesema kuanzishwa kwa
mashindano hayo yataweza kuhamasisha jamii kuhusu umuhimu wa unywaji wa kahawa
kama kinywaji cha afya na tamaduni na kwamba mashindano ya Kahawa Marathon si
tu yatakuwa fursa ya burudani, bali pia ni jukwaa la kuelimisha watu kuhusu
faida za kahawa," amesema.
"Tunataka kahawa kuwa sehemu
ya maisha ya kila siku kwa kuanzisha mashindano haya ya ‘Kahawaa Marathoni’ yatakwenda
kuleta burudani na elimu kwa wakati mmoja," amesema DC Kaji.
Mkuu huyo wa Wilaya amesema pamoja na kuhamasisha unywaji wa kahawa wa ndani, mashindano ya Kahawa Marathon yanaweza pia kusaidia kuongeza mapato kwa jamii, kuvutia washiriki na watalii na yataweza pia kutoa fursa za kibiashara zinazohusiana na zao la kahawa na hivyo kukuza uchumi wa eneo hilo.
Awali Mwenyekiti wa Kahawa
Festival 2024, Denis Mahulu, amesema idadi ya watu wanaoshiriki kuonyesha
bidhaa zinazotokana na zao la kahawa inazidi kuongezeka kila mwaka ambapo washiriki
kutoka maeneo mbalimbali, wamekuwa wakishiriki kuonyesha ubunifu na ubora
katika bidhaa zao.
Mahulu amesema kwamba
ongezeko la washiriki hao ni dalili nzuri ya ukuaji wa sekta ya kahawa, kupitia
Tamasha la Kahawa Festival-2024, wakati tamasha hilo linaanzishwa mwaka 2019 washiri walikuwa 25 na
kwa sasa washiriki wako zaidi ya 40, ambapo tamasha hilo, linatoa fursa kwa
wakulima na wazalishaji wa kahawa kuungana, kubadilishana mawazo, na kujifunza
mbinu bora za kilimo na usindikaji.
"Hii ni nafasi nzuri kwa
wakulima kuja kujifunza jinsi ya kuongeza thamani ya bidhaa zao na kufikia
masoko mapya," amesema.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa
Bodi ya Kahawa Tanzania (TCB), Primus Kimaryo, amesisitiza umuhimu wa matamasha
ya kahawa katika kusaidia wakulima wa zao hilo kupata mbinu bora za kilimo.
Amesema kuwa Tamasha la
Kahawa Festival-2024, linatoa jukwaa kwa wakulima kukutana na wataalamu wa
kilimo, ambapo wanaweza kupata mafunzo kuhusu mbinu za kisasa za kilimo,
usimamizi wa mashamba, na teknolojia mpya.
"Tunaamini kuwa elimu hii
ni msingi wa maendeleo. Wakulima wanapojifunza mbinu bora, wanakuwa na uwezo wa
kuongeza uzalishaji na kuboresha ubora wa kahawa yao," amesema Kimaryo.
Kimaryo ameongeza kuwa
matamasha yanaweza kusaidia kuboresha soko la kahawa nchini, kwa kutoa elimu na
mafunzo, wakulima wataweza kuzalisha kahawa bora, ambayo itavutia wanunuzi na
kuongeza thamani ya bidhaa za wakulima wa zao hilo katika masoko ya ndani na
nje.
Kauli Mbiu ya Kahawa Festival
2024 inasema; “Ushirikiano wa dau kwa Pamoja katika uendelezaji wa tasnia ya
Kahawa.”