Utekelezaji wa miradi ya EP4R yaanza kuleta mabadiliko ya maji Kilimanjaro

Meneja wa Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) Wilaya ya Moshi Vijijini Injinia Mussa Msangi, akizungumzia mafanikio ya utekelezaji wa miradi ya maji inayotekelezwa katika Wilayani humo  kupitia Programu ya Lipa Kulinagana na Matokeo (EP4R)

MOSHI-KILIMANJARO

Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vjijini (RUWASA) Mkoa wa Kilimanjaro, umeeleza mafanikio makubwa katika utekelezaji wa miradi ya maji, kupitia Programu ya Kulipa Kulingana na Matokeo (EP4R), ambapo miradi saba imekamilika kwa mwaka 2023/24.

Meneja wa Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWSA) mkoa wa Kilimanjaro Injinia Weransari Munisi, ameyasema hayo mnamo Septemba 2,2024 wakati akitoa taarifa kwa Mratibu wa programu ya Lipa kwa Matokeo (PforR) Mhandisi Mashaka Sitta, ambaye yuko katika ziara ya kikazi ya  ukaguzi wa miradi ya maji inayofadhiliwa na Benki ya Dunia mkoani humo.

Injinia Munisi amesema kuwa program hiyo imesaidia kuongeza upatikanaji wa maji hadi kufikia asilimia 82, huku miradi 13 ikiwa katika hatua mbalimbali za utekelezaji, ambapo ikikamilika inatarajiwa kuongeza kiwango cha upatikanaji wa maji kutoka asilimia 82 hadi kufikia asilimia 84. ifikapo Februari 2025.

Kwa upande wake Mratibu wa programu ya Lipa kwa Matokeo (PforR) Mhandisi Mashaka Sitta, amesisitiza lengo la miradi hiyo ni kuleta unafuu kwa wananchi.

Amesema kuwa mradi wa uboreshaji na upanuzi wa huduma ya maji katika Kata ya Kirua Vunjo Kusini utaanza kutoa huduma kwa wananchi ifikapo mwishoni mwa mwezi huu.

Awali  Mwenekiti wa Kijiji cha Yam-Makaa Omary Ally Mdee, amesema kukamilika kwa mradi huo maji utakwenda kutatua adha ya ukosefu wa maji ambayo imewakabili kwa miaka mingi wakazi wa kijiji hicho.

“Kwa ujumla, miradi hii inaonyesha jinsi ya kutumia rasilimali fedha kwa njia inayofaa ili kuboresha maisha ya wananchi na inatoa mfano mzuri wa jinsi ushirikiano kati ya Serikali na Wafadhili unavyoweza kuleta matokeo chanya.”amesema Mdee.

Nao baadhi ya wakazi wa Kitongoji cha Kiuo “B” kilichopo Kijiji cha Yam Makaa, Kata ya Kirua Vunjo Kusini Wilaya ya Moshi Vijijini, wameeleza furaha yao na matumaini makubwa yanayotokana na mradi huo wa maji.

Utekelezaji wa miradi ya Lipa kwa Matokeo (PforR) Mkoani Kilimanjaro ni mfano wa mafanikio ya kisiasa na kiuchumi katika kuhakikisha upatikanaji wa huduma bora za maji, na huenda ukatoa mwangaza wa matumaini kwa mikoa mingine nchini Tanzania.






Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.