Meneja wa Shirika la Posta Mkoa wa Kilimanjaro Bw. Abubakar Athumani, akizungumza na Waandishi wa Habari kuhusiana na Maadhimishi ya Siku ya Posta Duniani ambayo hufanyika Oktoba 9, ya kila mwaka.
MOSHI-KILIMANJARO.
Meneja wa Shirika la Posta
mkoani Kilimanjaro Abubakar Athuman, alisema masanduku ya posta (SLP) bado yana
umuhimu haswa ikitiliwa maanani ya kuwa Tanzania imeingia kwenye huduma
zinazohusiana na anwani za makazi.
Athuman amesema hayo Oktoba
9,2024 mjini Moshi, mkoani humo, wakati wa maadhimisho ya Siku ya Posta Duniani
kwa Mkoa wa Kilimanjaro, ambapo amesema ni vyema kila mtu, taasisi na hata
familia kuwa na anwani zao za masanduku ya posta.
Amesema pamoja na maendeleo
ya kiteknolojia ya kisasa bado masanduku ya posta yana umuhimu wake maana hata
ukitaka kusajili biashara yako moja wapo ya kigezo kinachohitajika ni anwani ya
sanduku la posta.
Aidha amesema kuwa
kuanzishwa kwa anawani za makazi kumerahisisha huduma za posta kutokana na
ukweli kuwa watu wengi kwa sasa wanapokea mizigo yao majumbani au maofisini
mwao moja kwa moja bila kuifika posta.
Amesema huduma ya anwani ya
makazi iliyoanzishwa na serikali hivi karibuni, kampuni ya posta wanaitumia
kama nyenzo muhimu ya kuwaunganisha na wateja wao.
Kwa upande wake msimamizi
wa kitengo cha barua Mkoa wa Kilimanjaro Veronica Magoto, amesema ni muhimu
kila mtu na hata taasisi kuwa na sanduku la posta kutokana na kuwa taarifa
nyingi zinazotoka serikalini zinahitaji huduma zinazohitaji masanduku ya posta
wakati wa mawasiliano.
Naye Afisa Postamasta mkoa
wa Kilimanjaro Charles Stephen, ametoa rai kwa Watanzania kujiunga na huduma za
duka la kimtandao ili waweze kujulikana na kukuza biashara zao.
Kauli mbiu ya mwaka huu ni miaka 150 ya kuwezesha mawasiliano katika kuboresha maisha ya watu duniani.







