Wafanyabiashara waaswa kutumia huduma ya duka mtandao kutangaza bidhaa

MOSHI-KILIMANJARO.

Wafanyabiashara na Wajasiriamali mkoani Kilimanjaro, wameasawa kutumia vyema wigo wa biashara ya huduma ya duka mtandao (Posta Online Shop) ili kuuza na utangaza bidhaa zao katika masoko ya ndani na nje ya nchi ili kukuza biashara zao.

Hayo yamesemwa mnamo Oktoba 9,2024 na Afisa Posta Masta Mkoa wa Kilimanjaro Charles Stephen, wakati akizungumza na Wafanyabiashara wa soko la Mbuyuni, lililopo katika Manispaa ya Moshi, ikiwa ni Maadhimisho ya Siku ya Posta Duniani, ambapo waliisherehekea kwa kuwatembelea wafanyabiashara hao na kuwaeleza umuhimu wa matumizi ya sanduku la Posta.

Akizungumzia huduma hiyo mpya, Afisa Posta Masta huyo amesema Shirika la Posta, limeanzisha huduma hiyo ili kuwasaidia wafanyabiashara na wajasiriamali kufanya biashara zao kwa njia ya mtandao.

Stephen, amesema mteja atakapojisajili kwa njia ya mtandao, ataweka bidhaa zake na maelezo kama bei, uzito na akishamaliza mteja huyo pia ataweza kuona bidhaa hizo kupitia duka  mtandao (Posta Online shop).

"Kupitia huduma ya duka mtandao (Posta Online Shop) mteja anaweza akanunua bidhaa kupitia huduma za kifedha za Tigo Pesa, M-Pesa, Airtel Money au kwa Credit Card na Shirika la Posta litaenda kuchukua hiyo bidhaa kwa muuzaji na kuipeleka kwa mteja moja kwa moja iwe ndani au nje ya nchi," amesema Stephen.

Aidha amesema mfanyabiashara au Mjasiriamali akijisajili kwenye huduma hiyo, atapata fursa ya kutangaza bidhaa zake kwenye wanachama 180 na kupitia Shirika la Posta, mteja anaweza akanunua bidhaa tofauti kwa wakati mmoja na akishalipia papo hapo alipo Posta itampelekea hadi nyumbani.

Katika hatua nyingine Postamasta huyo, ameupongeza Umoja wa Posta Afrika (PAPU) kwa kuendelea kuunga mkono juhuzi za Serikali kwenye Sekta ya Posta Barani Afrika hususan katika huduma za Kimtandao lengo likiwa ni kurahsisha huduma za Posta kwa wananchi.





 

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.