Mkuu
wa Wilaya ya Mwanga Bi. Mwanahamisi Munkunda, akijiandikisha kwenye Daftari la
Mpiga Kura kwa ajili ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa, katika Kitongoji cha Mwangondi kilichopo Mji Mdogo wa Mwanga, zoezi hilo limeanza Oktoba 11, 2024 nchi nzima na
litaendelea hadi Oktoba 20, 2024.MOSHI-KILIMANJARO
Serikali Wilayani Mwanga, mkoani Kilimanjaro, imesema kadi ya mpiga kura inayotolewa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) haitatumika katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa.
Mkuu wa Wilaya ya Mwanga Bi. Mwanahamisi Munkunda, ameyaesema hayo Oktoba 11,2024, wakati wa uzinduzi wa zoezi la uandikishaji kwenye daftari la Wapiga kura wa Serikali za Mitaa, lililofanyika kitongoji cha Mwangondi kilichopo mji mdogo wa Mwanga.
Bi. Munkunda ameeleza kwamba zoezi la kuandikisha wapiga kura, linaloendelea kuanzia Oktoba 11, 2024, linahusisha Uchaguzi wa Serikali za Mitaa utakaofanyika Novemba 27, 2024, na kuwataka wananchi kujitokeza kwa wingi ili waweze kuchagua viongozi wa vijiji na vitongoji.
Mkuu huyo wa Wilaya Amesisitiza kuwa mwananchi ambaye, hatajiandikisha hatapata fursa ya kushiriki katika uchaguzi huo.
Amesema kuwa Tume ya Taifa ya Uchaguzi inafanya uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga kura kwa ajili ya uchaguzi wa Rais, Wabunge, na Madiwani, na kwamba uchaguzi wa Serikali za Mitaa unasimamiwa na Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI).
Awali akizungumza Msimamizi wa Uchaguzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mwanga, Wakili Edwin Lusa, amesema watu 64,500 wanatarajiwa kuandikishwa kwenye daftari la wapiga kura kwa Uchaguzi wa Serikali za Mitaa, utakaofanyika Novemba 27, 2024, huku jumla ya vituo 291 vya kujiandikishia vitafunguliwa kuanzia saa mbili kamili asubuhi na kufungwa saa kumi kamili jioni.
Naye Mwenyekiti wa kitongoji cha Mwangondi, Henry Chaki, amesema wananchi wamepokea zoezi la uandikishaji kwa ari kubwa na wengi wamehamasika kujiandikisha kwenye daftari la orodha la wapiga kura.
Chaki ameongeza kuwa juhudi hizo ni muhimu kwa ajili ya kuhakikisha kwamba wananchi wanapata fursa ya kushiriki katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa.
Uchaguzi
wa Serikali za Mitaa wa kwa mara ya mwisho ulifanyika Novemba 2019, na uchaguzi
wa Serikali za Mitaa mwaka 2024 unatarajiwa kufanyika Novemba mwaka huu.
Mkuu wa Wilaya ya Mwanga Bi. Mwanahamisi Munkunda, akiwahamasisha wananchi kujitokeza kujiandikisha kwenye daftari la mpiga kura kwa ajili ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa.
Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya Mwanga Bi. Zahara Msangi, akijiandikisha kwenye daftari la mpiga kura kwa ajili ya uchaguzi wa Serikali za mitaa utakaofanyika mwezi Novemba mwaka 2024


