Watu 1,360 mwanga hawajui kusoma wala kuandika

Afisa Elimu Watu Wazima Halmashauri ya Wilaya ya Mwanga Mwl. James Tesha, akisoma risala ya kilele cha Maadhimisho ya Juma la Elimu ya Watu Wazima Ngazi ya Wilaya yaliyofanyika katika Chuo cha Ufundi Stadi MALAGE VTC.

MWANGA-KILIMANJARO

Zaidi ya watu 1,360 Wilayani Mwanga Mkoani Kilimanjaro hawajui kusoma, kuandika wala kuhesabu wengi wao wakiwa wa maeneo ya vijijini jambo ambalo linaashiria kwamba kuna haja ya kuhamasisha elimu ya watu wazima maeneo hayo.

Hayo yamesemwa na Afisa Elimu Watu Wazima Halmashauri ya Wilaya ya Mwanga Mwl. James Tesha, wakati akisoma risala ya kilele cha Maadhimisho ya Juma la Elimu ya Watu Wazima Ngazi ya Wilaya, yaliyofanyika katika Chuo cha Ufundi Stadi MALAGE VTC.

Amesema kati ya watu hao wasiojua kusoma na kuandika wanaume wako 490 na wanawake 870 na hivyo kufikisha idadi ya watu wasio jua kusoma na kuandika 1360.

Amesema wanafunzi 14 waliokuwa wanasoma madarasa ya memkwa walifanya mtihani na kujiunga na elimu rasmi, huku walimu 47 waliojiendeleza kupitia elimu ya masafa waliweza kufaulu na kupata Stashahada.

Amesema kupitia programu ya elimu ya masafa (ODL) walimu wapatao 47 waliweza kujiendeleza kutoka ngazi ya Astashahada kwenda Stashahada bila kuadhili kazi na wengine wanaendelea kujiunga.

Aidha amesema halmashauri ya Wilaya ya Mwanga ina vyuo vya ufundi vinavyomilikiwa na mashirika na watu binafsi, ambapo vyuo hivyo hutoa fursa kwa wanafunzi waliokosa nafasi ya kuendelea na elimu ya mfumo rasmi.

Amesema changamoto iliyojengeka katika jamii ni kuwa na fikra kwamba elimu ya watu wazima ni kujifunza kusona na kuandika tu na hiyo imepelekea jamii kushindwa kukitumia kitengo cha elimu ya watu wazima.

Diwani wa Kata ya lembeni Alexs Mwaipopo ameomba maaeneo yote ya taasisis za serikali kupimwa na kutoa hati miliki kwa wahusika ili kuepusha mvutano na migongano ya kimasilahi ambayo imekuwa ikijitokeza kutokana na mtu au watu kuvamia na kujimilikisha maeneo ya serikali kinyemera.

Afisa Elimu Divisheni ya Sekondari Wilaya ya Mwanga Reuben Mnzava, amesisitiza shule zote za sekondari wilayani huo kuanzisha program ya ujasiriamali  kwani elimu ya ujasiriamali ni muhimu katika ngazi zote ambayo humuandaa kijana juu ya maisha yake ya baadaye.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mwanga Zahara Msangi, ameishukuru serikali kwa kuweza kujenga vyuo vya ufundi nchi nzima, ikiwemo wilaya ya Mwanga.

Kwa mujibu wa Sensa ya Watu na Makazi ya Mwaka 2022 Wilaya ya Mwanga ina jumla ya Wakazi 14,8763 wakiwemo Wanawake 76,606 na Wanaume 72,157, huku watu wasiojua kusoma wala kuandika wakiwa 1,360, wanaume wakiwa 490 na wanawake 870.










Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.