Msimamizi wa Uchaguzi
Serikali za Mitaa Wilaya ya Mwanga Wakili Edwin B. Lusa, akitoa maelezo ya
uchaguzi Serikali za Mitaa, kwa wananchi walioshiriki mkutano huo ulichofanyika
katika uwanja wa CD Msuya.
MWANGA-KILIMANJARO.
Halmashauri ya Wilaya
ya Mwanga, mkoa wa Kilimanjaro, imetoa maelekezo ya uchaguzi Serikali za Mitaa
unatakaofanyika Novemba 27 mwaka huu.
Maelekezo ya uchaguzi
huo, yanalenga kuwapata Wenyeviti wa Mitaa na Wajumbe Watano wa Kamati za Mitaa
katika Mamlaka za Miji na Vijiji.
Akizungumza katika
mkutano huo uliofanyika katika uwanja wa CD Msuya, Msimamizi wa uchaguzi wa
halmashauri hiyo Wakili Edwin Lusa, amesema lengo ni kuhakikisha Taratibu zote
za Uchaguzi zinafuatwa, lakini pia wagombea na wapiga kura wanapata taarifa
zote zinazohitajika kwa wakati.
“Maelekezo haya
yanafafanua hatua zitakazoongoza mchakato mzima wa uchaguzi, kuanzia
uandikishaji wa wapiga kura, uchukuaji na urejeshaji wa fomu za kugombea,
uteuzi wa wagombea na tarehe ya siku ya uchaguzi,”amesema wakili Lusa.
Aidha amesema
maelekezo mengine ni yale yanayohusu kutoa
mwongozo ili kuhakikisha uchaguzi unafanyika kwa uwazi, haki na usawa na kwa
kuzingatia Sheria na Taratibu zilizowekwa.
Pia Wakili Lusa amesema
wanaoruhusiwa kugombea nafasi za Wenyeviti na Wajumbe ni Watanzania wenye umri kuanzia miaka 21 na
kuendelea huku wanaoruhusiwa kupiga kura ni wananchi wenye umri wa miaka 18 na
kuendelea na ambao walishiriki na watakaoshiriki zoezi la uandikishaji wa
wapiga kura.
“Nitoe wito kwa Wananchi
wote wenye sifa, kushiriki kikamilifu katika mchakato huu wa uchaguzi, kuanzia
hatua ya kujiandikisha kwenye orodha ya wapiga kura, kujiandikisha katika
orodha ya wapiga kura ni hatua muhimu inayompa
kila mwananchi mwenye sifa haki ya Kisheria ya kushiriki uchaguzi kama mpiga kura au mgombea.”amesema.
Kwa upande wake
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mwanga Zahara Msangi, amesema
kufanyika kwa uchaguzi wa Serikali za Mitaa kunawezesha wananchi kutumia haki
yao ya Kikatiba ya kuomba kuongoza wenzao na kuchagua viongozi wa maeneo
wanayoishi.
“Uchaguzi huu una
hatua mbalimbali ambazo ni wananchi kujiandikisha kwenye daftari la orodha ya
wapiga kura na mwisho kushiriki kwenye zoezi la uchaguzi.
Aidha wale wote wenye sifa za kugombea nafasi mbalimbali za uongozi kuomba nafasi hizo kupitia udhamini wa vyama vyao vya kiasiasa.
Mkurugenzi mtendaji wa
Halmashauri ya Wilaya ya Mwanga Zahara A. Msangi, akitoa maelezo ya uchaguzi wa
Serikali za Mitaa, hafla iliyofanyika katika uwanja wa CD Msuya Wilayani humo.


Wakuu wa Idara wakifuatilia kwa makini maelekezo ya uchaguzi wa Serikali za Mitaa, yaliyokuwa yakitolewa na Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mwanga Zahara Msangi.


Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Mwanga Mwl. Ibrahim Mnzava (Kushoto) akiteta jambo na Mwenyekiti wa UVCCM Wilayani humo.
