MUWSA yapongezwa kwa kujenga maabara ya ubora wa maji


MOSHI-KILIMANJARO

Maabara za ubora wa maji ni eneo muhimu katika kuhakikisha huduma ya maji wanayopatiwa wananchi inakuwa salama kwa matumizi yao.

Serikali kupitia Wizara ya Maji, ndio inayosimamia maabara za maji kwa nchi nzima ambazo, zimegawanyika katika mikoa mbalimbali.

Akitoa taarifa ya utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa Maabara ya ubora wa Maji kwa Kamati ya Siasa mkoa wa Kilimanjaro Mkurugenzi wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Mjini Moshi Mhandisi Kija Limbe amesema (MUWSA) ilianza utekelezaji wa ujenzi wa maabara hiyo Agosti 2024 na kukamilika Aprili, 2024.

Mhandisi Limbe amesema awali mamlaka hiyo, ilikuwa na maabara ndogo kwa ajili ya ubora wa Majisafi, kutokana na Mamlaka hiyo kuongezewa maeneo ya kutoa huduma , waliamua kubuni mradi wa ujenzi wa maabara kubwa itakayokidhi mahitaji yanayoendana na ongezeko hilo.

“Zaidi ya wateja 58,246 wanaoishi katika Manispaa ya Moshi na maeneo ya Moshi Vijijini yanayo hudumiwa na MUWSA, hivyo tuna hakikisha wateja wote hawa wanapata huduma ya majisafi na salama kwa ajili ya kuboresha afya zao,” amesema.

Amesema mradi huo mpaka kukamilika kwake umegharimu kiasi cha Sh milioni 81.8 inayojumuisha gharama za ujenzi wa jengo pamoja na ununuzi wa vifaa vya maabara na fedha hizo ambazo zimetumika kugharamia ujenzi wa maabara hiyo ni fedha kutoka mapato ya ndani.

“Utekelezaji wa mradi huu umekamilika kwa asilimia 100, ikiwemo ujenzi wa jengo la maabara, ujenzi wa mtaro wa kudhibiti maji ya mvua na ufungaji wa vifaa vya maabara na kwamba Mamlaka hiyo iko kwenye mchakato wa kuendelea kununua vifaa vingine vya maabara,”amesema Mhandisi Limbe.

Mwenyekiti wa CCM MKoa wa Kilimanjaro Patrick Boisafi, amempongeza Mkurugenzi wa (MUWSA) na timu yake kwa kubuni mradi huo ambao utakwenda kuwanufaisha wananchi wa Manispaa ya Moshi na maeneo mengine kwa kupata huduma bora na endelevu ya Majisafi na salama.

Awali akizungumza Mstahiki Meya wa Manispaa ya Moshi Injinia Zuberi Kidumo, amesema viko baadhi ya vijiji bado vinatumia maji ya visima na kuiomba Mamlaka hiyo, kutoa elimu zaidi hususani maeneo ya vijijini, kabla hawajaanza kuyatumia maji hayo wawze kuja kupima maji hayo ili kujua usalama wake zaidi.

Naye Mbunge wa Jimbo la Moshi Mjini Priscus Tarimo, amesema yako maeneo ambayo watu bado wanaharibu mazingira kwa kuchota mchanga kwenye mito na kutoa mawe kwa ajili ya kuponda kokoto na hivyo  kusababisha vyanzo vya maji kupungua.

“Niwaombe MUWSA badala ya kuwafukuza kwa Sheria watu hao ni vizuri  MUWSA ikawatafutia shughuli mbadala kwa kutumia CSR inayopatikana kwenye mamlaka hiyo ili waweze kuondokana na uharibifu huo wa kimazingira kwenye mito,”amesema Mbunge Tarimo.

Akitoa maelezo ya namna maabara hiyo inavyofanya kazi Fundi sanifu Mwandamizi kutoka MUWSA Joseph Revocatus, amesema maabara ya ubora wa maji ni maabara maalumu ya kupima maji ili kuona kemikali zilizopo ambazo zinaweza kuzidi au kupungua kukawa na madhara kwa binadamu pamoja na viumbe hai kwenye mwili wa binadamu.

“Maabara hii inauwezo wa kuchukua sampuli zisizo pungua 56, ingawa tumejiwekea kuchukua vipimo vya sampuri 48, ambapo tumeweka vituo kwenye maeneo yote ambayo tunayahudumia, ikiwemo kwenye taasisi za elimu, vilula, masoko, vyanzo vya maji na kwenye matanki ili kujua ubora huo wa maji,”amesema mtaalamu huyo wa maabara ya ubora wa maji.

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro Nurdin Babu, ameupongeza uongozi wa MUWSA kwa kufanya  utafiti  ambao umewezesha kujenga maabara hiyo ya ubora wa maji.

Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira MUWSA ndio Mamlaka bora Tanzania kwa miaka mingi inaongoza kwa kutoa huduma bora za maji.

















Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.