Manispaa ya Moshi yapokea Sh bilioni 1.8 ujenzi Hospital ya Ghorofa

MOSHI-KILIMANJARO

Halmashauri ya Manispaa ya Moshi, imepokea kiasi cha Sh Bilioni 1.8 kutoka Serikali Kuu kwa ajili ya ujenzi wa Hospitali ya Wilaya ya ambayo inajengwa kwa majengo ya kwenda juu (ghorofa) eneo la Msaranga Kata ya Ng’ambo ili kupambana na changamoto ya ufinyu wa eneo.

Hayo yamo kwenye taarifa ya Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Manispaa ya Moshi Mwajuma Nasombe, aliyoisoma Septemba 25,2024 kwa Kamati ya Siasa ya Chama cha Mapinduzi (CCM) iliyotembelea na kujionea maendeleo ya ujenzi wa hospital hiyo.

Mwl. Nasombe amesema katika mwaka wa fedha 2021/2022 na 2022/2023 Halmashauri hiyo ilipokea kiasi cha Sh Bilioni 1.8 kati ya fedha hizop kiasi cha Sh bilioni 1.2. zimekwisha kutumika na kwamba hatua ambayo inayoendelea kwa sasa katika mradi huo ni kukamilisha slub kwa ghorofa ya chini na kusuka nguzo kwa ajili ya ghorofa ya kwanza, ambapo hadi kukamilika kwake utagharimu kiasi cha Sh Bilioni 6.5

Akizungumza Mstahiki Meya wa Manispaa ya Moshi Mhandisi Zuberi Kidumo, amesema lengo la Manispaa kujenga hospitali ya Wilaya ilikuwa ni kupunguza msongamano wa wagonjwa katika hospitali ya rufaa ya mkoa Mawenzi na kwenye hospitali ya Kanda ya Kaskazini KCMC.

“Tunaishukuru sana Serikali kwa kuweza kutuletea fedha hizi kwa ajili ya ujenzi wa hospitali ndani ya Manispaa yetu, kukamilika kwa hospitali hii, itakwenda kutatua changamoto za wananchi kuweza kupata huduma karibu na maeneo yao,”amesema Mhandisi Kidumo.

Naye Mbunge wa Jimbo la Moshi Mjini Priscus Tarimo, amesema “Serikali ilitutaka tuwe na heka 20 mpaka 50 ndipo iweze kutoa fedha za kujenga hospitali, kwa sasa hospitali inapojengwa ni eneo lenye heka sita tu, naishukuru sana Serikali kwa kukubali kutoa fedha za kujenga hospitali hii kwa ghorofa,”amesema Tarimo.

Ameongeza kusema “Ni kweli kabisa Serikali kama ingeweza kusimia miongoza ya Wizara ya Afya kama inavyotaka, leo hii tusingeweza kupata fedha za kujenga hospitali kwenye  eneo lenye heka sita.”

Kwa upande wake Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Kilimanjaro Patrick Boisafi ampongeza Mbunge  Priscus Tarimo, kwa ushawishi wake mkubwa Bungeni na kuweza kufanikisha kujenga hoja Serikalini na ikakubali kutoa fedha kwa ajili ya kujengwa kwa hospitali hiyo.

“Ni kweli mkoa wetu wa Kilimanjaro tuna changamoto ya ufinyu wa ardhi, Kamati ya Siasa ya mkoa inakupongeza sana Mbunge kwa kutengeneza ushawishi, wakaielewa hoja yako, wakakuunga mkono na ndio maana Serikali imetenga Sh bilioni 6.5 kwa ajili ya ujenzi wa hospitali hii”.








Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.