HAI-KILIMANJARO.
Wajumbe wa Kamati ya Siasa
ya Chama cha Mapindizi (CCM) Mkoa wa Kilimajaro, wameipongeza Halmashauri ya
Wilaya ya Hai kwa utekelezaji mzuri wa Ilani ya CCM ya mwaka 2020-2025, ambapo
imeweza kutenga fedha zinazotokana na mapato yake ya ndani na kujenga Kituo cha
Afya Masama Kati.
Hayo yamejiri Septemba 24,
2024, wakati wa ziara ya Kamati ya Siasa mkoani humo, ilipotembelea na kukagua mradi
wa ujenzi wa Kituo cha Afya Masama Kati,
unaotekelezwa kwa mapato ya ndani ya halmashauri hiyo kwa gharama ya SH milioni
209.
Akizungumza mara baada ya kukagua ujenzi wa kituo hicho, Katibu wa CCM mkoa wa Kilimanjaro Mercy Mollel, ameipongeza Halmashauri hiyo kwa kuwa kinara wa ukusanyaji wa mapato ya ndani fedha ambazo zimewezesha kujenga kituo hicho cha afya.
“Nikupongeze Mwenyekiti wa Halmashauri ya Hai, Mkurugenzi mtendaji na Wataalamu kwa kusimamia vizuri ukusanyaji wa mapato ya ndani, fedha ambazo zimewezesha kujenga kituo hiki cha afya kupitia mapato yenu ya ndani,”amesema Mollel.
Aidha amesema Serikali ya
Awamu ya Sita imeamua kuwasogezea karibu wananchi wake huduma za afya karibu na maeneo ya wananchi.
Akisoma taarifa ya mradi wa
ujenzi wa Kituo kipya cha afya Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Wilaya ya Hai
Dkt. Itikija Msuya, amesema hadi
kukamilika kwa mradi huo utagharimu kiasi cha Sh milioni 209 ambapo hadi
sasa zaidi ya Sh milioni 125 zimekwisha
kutumika.
Awali Mwenyekiti wa
Halmashauri ya Wilaya ya Hai, Edmund Rutaraka, amesema mapato ya ndani, yamezidi
kuongezeka kutoka Sh bilioni 4.2 mwaka 2022/2023 hadi kufikia Sh Bilioni 4.5 mwaka
2023/2024.
Diwani wa Kata ya Masama
Kati Kandata Kimaro, amesema akina mama wajawazito, walikuwa wakijifungulia
njiani kutokana na kukosa huduma za matibabu karibu na eneo hilo.
Katibu Tawala Mkoa wa
Kilimanjaro Yusuf Nzowa, amewataka wananchi na watendaji, kuhakikisha kwamba
wanailinda na kutunza miundombinu yote inayotekelezwa na Serikali wilayani humo.
“Litakuwa ni jambo la
kusikitishasana kama tutasikia miundombinu hii inahujumiwa, tuhakikishe
tunailinda kwani serikali imewekeza fedha nyingi na tuipe thamani inayostahili”
amesema Nzowa.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Hai
Lazaro Twange amesema, melekezo yaliyotolewa na Wajumbe wa Kamati ya Siasa ya
CCM Mkoa, wameyapokea na kwamba watayafanyia kazi kwa wakati, ikiwemo la
kufunguliwa kwa barabara yenye urefu wa kilomita 1.6 ili iweze kupitika kwa
muda wote kufika katika kituo hicho cha afya.
Kwa mujibu wa Sensa ya Watu na makazi ya Mwaka 2022 Kata ya Masma Kati ina jumla ya Wananchi 12,000, hivyo kukamilika kwa mradi huo utakwenda kutatua changamoto ya upatikanaji wa huduma za afya ngazi ya kiytuo cha afya kwenye kata hiyo.














