
Majengo ya Kituo Kipya cha Afya Holili, yaliyojengwa na Serikali Kuu
ROMBO-KILIMANJARO.
Kamati ya Siasa ya Chama cha Mapinduzi CCM Mkoa wa Kilimanjaro, imeagiza Kituo kipya cha Afya Holili kilichopo Kata ya Holili Wilaya ya Rombo kianze kufanya ifikapo Septemba 30 mwaka huu, baada ya majeengo kukamilika, hatua ambayo itawaondolea wananchi kutembea umbali mrefu kufuata matibabu.
Katibu wa CCM Mkoa wa Kilimanjaro Mercy Mollel, ametoa agizo hilo Septemba 23,2024 baada ya Kamati hiyo kutembelea na kukagua miradi ya maendeleo inayotekelezwa na Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan Wilayani Rombo.
Kamati ya Siasa inatoa muda wa siku saba, kituo hicho kianze kutoa huduma za matibabu ili wananchi wa kata hiyo waanze kupata huduma za matibabu katika kituo hicho.
Aidha Kamati hiyo imempongeza Mkuu wa Wilaya ya Rombo Mwl. Raymond Mangwala na timu yake kwa usimamizi mzuri wa ujenzi wa mradi huo, ambao umegharimu zaidi ya Sh milioni 500 hadi kukamilika kwake na kuomba miundombinu hiyo iweze kutunzwa.
Akizungumzia changamoto ya barabara
iliyowasilishwa na Diwani wa Kata ya Holili Kelvine Kahangala, Katibu huyo
ametoa maelekezo kwa Meneja wa Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA)
kuona namna ya kuweza kusaidia kuitengeneza barabara ili iweze kutumika kwa
muda wote.
Akisoma risala ya ujenzi wa Kituo hicho msimamizi wa mradi huo Mhandisi Luis Sunga, amesema kitu hicho kilipokea Sh milioni 500 kwa ajili ya ujenzi wa jengo la upasuaji, wodi ya Wazazi, maabara na jengo la kuhifadhia maiti na Sh milioni 140 kwa ajili ya kununua vifa tiba.
Amesema baada ya kukamilia ujenzi huo, jumla ya Sh milioni 53 zilibaki ambapo zitatuka kwa ajili ya ununuzi wa kiyoyozi, kulipa vioo vya venti za milango,kulipa vifaa vya kuingizia maji ndani ya majengo, kujenga njia za kupitia wagonjwa na kuimarisha mifumo ya maji safi kwa kujenga minara miwili ya maji na matenki ya maji lita 10,000.
Awali akizungumza Diwani wa Kata hiyo Kelvine Kahangala amesema licha ya Serikali kuwekeza fedha nyingi za ujenzi wa miundombinu ya afya na elimu, changamoto kubwa iliyopo kwa sasa ni ubovu wa barabara inayomuwezesha mgonjwa kufika katika kituo hicho kupata huduma za matibabu.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Rombo Raymond Mangwalla, amesema zaidi ya Sh bilioni 62, zimeletwa na Serikali kuu Wilayani humo kwa ajili ya shughuli za maendeleo, ambapo katika sekta ya maji imepokea kiasi cha Sh biloni 22, sekta ya elimu na afya cha Sh bilioni 26, huku TARURA ikipokea kiasi cha Sh bilioni 14.
Kamati ya Siasa mkoa, imetembelea ujenzi barabara ya Holili-Tarakea-Nayemi inayojengwa kwa kiwango cha lami, ujenzi wa bwalo la wanafunzi shule ya sekondari Mashati, Kituo cha afya Mkuu, ukumbi wa , Wodi ya wazazi na ujenzi wa barabara ya Bus Stand-Magereza.
Kamati ya Siasa ya Chama cha Mapinduzi (CCM)Mkoa ikikagua majengo ya Kituo cha Afya Holili, wa pili kulia ni Katibu wa CCM mkoa wa Kilimanjaro Bi. Mercy Mollel, wa kwanza kulia ni Mjumbe wa Kamati ya Siasa mkoa Chifu Babu Daud Mrindoko.





