Timu ya Endumet FC, ikifanya mazoezi kabla ya kuanza kwa mechi yake ya kirafiki na Timu ya Polisi Tanzania, ikiwa ni uzinduzi wa uwanja huo.
ENDUMET-SIHA
Mnamo mwaka 2021 Rais Samia Suluhu Hassan alifungua Barabara ya Sanya Juu Hadi
Elerai ambayo ipo kwenye kiwango cha lami.
Hafla hiyo ilifanyika eneo maarufu sana la Dutch Corner karibu na makao makuu
ya Wilaya ya Siha mkoani Kilimanjaro, na kuhudhuriwa na mamia ya wakazi wa
Sanya Juu na Siha kwa ujumla wake.
Wenyeji wa vijiji ambavyo barabara hiyo imepita ikiwamo Matadi, Ngarenairobi na
Miti Mirefu walikuwa miongoni mwa waliotupia macho uzinduzi huo muhimu kwa
wakazi wa West Kilimanjaro na viunga vyake.
Miongoni mwa waliokuwapo katika hafla hiyo alikuwapo Baltazar Momoya ambaye ni
Mwekezaji katika eneo la West Kilimanjaro huku maskani yake yakiwa Matadi.
Baltazar Momoya ambaye ni maarufu sana kwa eneo hilo kwa jina la BRM alianza
kama mchicha katika maisha yake hadi kufikia uwekezaji mkubwa katika viwanda
vya kuchakata mazao ya misitu na kilimo.
Ambapo changamoto mbalimbali amezishuhudia ikiwamo katika sekta ya michezo
ambapo kwa muda mrefu kiu yake ya ilikuwa ni kutaka kusaidia watu wa eneo lake
na vijiji vya karibu.
Oktoba 2021 Rais Samia
Suluhu Hassan aliposema uwepo wa barabara ya lami katika eneo hilo utafungua
njia kwa wazawa na taifa kwa ujumla.
BRM alikunwa kisawasawa na kauli ya Rais Samia na kuonyesha hilo, alienda mbali
zaidi katika suala la michezo pale Rais alipotamka mpango wa ujenzi wa uwanja
unaondelea jijini Arusha ambao utatumika katika Michuano ya AFCON mnamo mwaka
2027.
Mwekezaji huyo amenunua ekari 50 katika Kijiji cha Roseline ambapo uwekezaji
wake umejikita katika Soka ambapo ameanza na uwanja katika eneo la kuchezea
ambalo limezingatia viwango vya kimataifa.
Hatua hiyo BRM ameona fursa kubwa wakati na baada ya AFCON 2027 kwamba utazidi
kufungua eneo hilo la West Kilimanjaro kutokana na uwanja huo kuwa katikati ya
milima miwili maarufu nchini na Afrika ya Kilimanjaro na Meru.
"Kupenda kwangu masuala ya michezo na kusaidia watu wanaonizunguka ndio
sababu ya kujitosa kununua eneo la ekari 50 ili kupanua wigo wa wawekezaji
wazawa nchini," alisema Baltazar.
Mbali na hilo BRM amekuwa mfano kwani amefanikiwa kuanzisha timu inayofahamika
kwa jina la Endumet FC ambayo anaamini siku moja itacheza Ligi Kuu Tanzania
Bara ambapo kwa sasa ipo Ligi daraja la tatu mkoani Kilimanjaro.
"AFCON inakuja, binafsi nimeona fursa hiyo walau nipate hata timu moja
itayokuja kupiga kambi hapa; nimeanza ujenzi katika hatua ya eneo la
kuchezea," aliongeza Baltazar
Hata hivyo Baltazar aliwataka wakazi wa eneo hilo kutambua kuwa mpira sio vita
wala uadui isipokuwa ushirikiano na kuvumilia kutaijenga Mjimwema, Siha na
taifa kwa ujumla.
Uwepo wa eneo zuri na bora la kuchezea unatia hamasa kwa wachezaji kufanya
vizuri pia unavutia timu nyingine kwenda kuchezea katika dimba hilo, lililopo
katika Kijiji Roseline huko Mjimwema.
Mnamo Septemba 9, 2024 Uwanja huo ulizinduliwa na Diwani wa Kata ya Ndumeti
Vicent Kileo "Jambo lililofanyika na ndugu yetu Baltazar Momoya, ni Jambo la kuigwa, ni
Jambo la kihistoria katika kata, Wilaya," alisema Kileo.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Chama Cha Soka Wilaya ya Siha Hassan Karata
alisema haijawahi kutokea katika Wilaya ya Siha uwekezaji mkubwa uliofanywa na
Baltazar Momoya.
Mashabiki walioshuhudia uzinduzi huo waliongeza kuwa uwekezaji wa uwanja
utafungua fursa hivyo ni jukumu la vijana kuchangamkia fursa hizo.
"Tunamshukuru Mungu kwa Baltazar, BRM; hatujawahi kuona Mjimwema
pamebadilika kiasi hiki; Tunamshukuru Mungu alivyomuonyesha Baltazar fursa
hii," alisema Prisila Mwakajila.
Tanzania itakuwa mwenyeji wa fainali za AFCON 2027 ambapo miji ya Dar es
Salaam, Dodoma, Arusha na Zanzibar itapata fursa ya viwanja vya Soka.






