MOSHI-KILIMANJARO
Watoto nchini wametakiwa kujilinda, kujitambua na kujithamini katika masuala mbalimbali yanayohusu malezi na makuzi yao sambamba na kutoa taarifa pale wanapofanyiwa vitendo vya unyanyasaji wa kijinsia.
Hayo yameelezwa na Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Ushirika Moshi (MoCU) Beatrice Kimaro, wakati akifundisha Program ya Watoto Mentorship Adventure, ambayo ilikuwa inahusu watoto kujitambua, iliyoandaliwa na Shirika lisilo la kiserikali la Inspire Change lililopo mjini Moshi mkoani Kilimanjaro.
Amesema kutokana na matukio mbalimbali ya kijinsia mabayo yanaendelea kutokea kwenye jamii, yakiwemo ya maswala ya ulawiti na ubakaji, amewaasa watoto hao kupinga vitendo hivyo kwa kuvitolea taarifa kwenye dawati la polisi ili kuweza kufikia malengo yao ya maisha.
“Kutokana na matukio ya ukatili ambayo yanaendelea kwenye jamii yakiwemo maswala ya ukatili kwa watoto, ulawiti na ubakiji, lakini wanapokutana na changamoto kama hizi kuona namna ya kukabiliana nazo ikiwa ni pamoja na kutoa taarifa kwa jeshi la polisi kitengo cha dawati,”
Aidha amesema mabadiliko ya maisha yamewafanya wazazi wengi kutingwa na kazi kiasi cha kuacha majukumu ya kulea watoto kuwa ya wafanyakazi wa ndani.
“Watoto wengi kwa sasa wanalelewa na dada wa kazi (House Girl) au Bibi na Babu, huku wazazi wakikimbizana na maisha ya kutafuta pesa nah ii imekuwa ni changamoto kubwa inayoikabili jamii kwa sasa ya wazazi kuweka kazi kwanza na sio mtoto kwanza,”amesema Mhadhiri huyo Kimaro.
Amesema hali hiyo inafanya jukumu la kuwalea watoto liachwe kwa akina dada ambao wengi wao hutoka vijijini katika mazingira na utamaduni tofauti kuja kufanya kazi maeneo ya mijini.
“Akina dada wa kazi ndio wamekuwa wazazi wa watoto hawa kwani hufanya kazi zote kuanzia kuwaamsha asubuhi, kuwaogesha, kuwapeleka shule, na hata wakirudi shuleni huwapokea na kuwapa chakula , huzungumza nao na huo ndio umekuwa mtindo wa maisha ya kila siku,”amefafanua.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa shirika lisilo la kiserikali la Inspire Change Wakili Haika Harrison Ngowi, amesema malezi ya mzazi ni bora kwa watoto na kwamba yana tija kwa ajili ya kumkuza mtoto katika misingi ya maadili mema.
“Changamoto kubwa iliyopo kwa sasa ni malezi ya watoto, wazazi wengi hawana muda kuwafuatilia watoto wao, wako bize kutafuta pesa, hawana mahusiano mazuri na watoto wao hata malezi ya watoto wao yamekuwa sio sahihi, hivyo ninawaasa wazazi kubeba jukumu la malezi ya watoto wao ili kuja kuwa na kizazi bora,”amesema Wakili Ngowi.
Aidha amesema kutokana na changamoto ya ukatili iliyopo kwa sasa Shirika la Inspire Change, limeanzisha Program ambayo inaitwa Watoto Mentorship Adventure ili kuwafundisha watoto kuhusiana na maswala ya kupinga ukatili lakini pia kuweza kujitambua wao ni akina nani.
Akifungua warsha hiyo ya siku tatu kwa niaba ya Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya Manispaa ya Moshi Mwajuma Nasombe, Mkuu wa idara ya elimu Divisheni ya Sekondari Alberta Makule, amesema kumekuwepo na wimbi kubwa la watoto kutelekezwa na wazazi wao huku wengine wakipewa majukumu makubwa ya kulea familia.
Aidha ameipongeza Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa kuweka mfumo wa pamoja wa uanzishwaji, uendeshaji na ufuatiliaji wa Dawati la Jinsia ambalo limekuwa likihakikisha watoto hawatendewi ukatili.