Tahadhari ya homa ya nyani yatolewa kwa wananchi Siha

 SINAI-SIHA

Wananchi Wilayani Siha Mkoani Kilimanjaro, wametakiwa kuendelea kuchukua tahadhari juu ya ugonjwa wa homa ya nyani ambao unaosababishwa na kirusi aina ya Mpox.

 

Kauli hiyo imetolewa na Mkuu wa Wilaya ya hiyo Dkt. Christopher Timbuka, wakati akizungumza na wananchi wa kijiji cha Sinai na Darajani vilivyopo wilayani humo wakati wa hafla fupi ya kukabidhi hati miliki za ardhi kwa wananchi takribani 523 waliokubali kurasimisha maeneo yao.

 

Amesema kila mtu kwa nafasi yake anapaswa kuchukua tahadhari kwa kutoa elimu kwa jamii huku akiwasihi wananchi kuzingatia elimu ambayo inatolewa na wataalamu wa afya ikiwa ni pamoja na kuendelea kunawa mikono kwa maji tiririka, kupunguza watu kusalimiana kwa kushikana mikono ili ugonjwa huo usiingie ndani ya wilaya hiyo na nchi kwa ujumla.

 

Aidha Mkuu huyo wa Wilaya amewataka Wataalamu wa Afya kuendelea kutoa elimu kwa jamii  kuhusu dalili na namna ya kujikinga na ugonjwa huku akiwaomba viongozi wa dini kushirikiana na serikali kutoa elimu kwa waumini wao kwenye nyumba za ibada.

 

Katika kuhakikisha kuwa wanafunzi wa msingi na sekondari wanakuwa makini katika ujifunzaji wawapo shuleni hususa ni nyakati za mchana, wazazi wameombwa kuwezesha upatikanaji wa chakula cha mchana shuleni ili wanafunzi waweze kujifunza kwa utullivu.

 

Vilevile mkuu huyo wa Wilaya amewataka wananchi kuendelea kupinga vitendo ya ukatili kijinsia kwa wanawake na watoto vinavyoendelea kwenye maeneo yao wanayowazunguka.








Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.