MOSHI-KILIMANJARO.
Mwenyekiti wa Chama cha
Mapinduzi (CCM) Moshi Mjini Faraji Swai, amewataka Wananchi wa Manispaa ya Moshi
mkoani Kilimanjaro, wanapotaka kununua ardhi, kufuata taratibu kwa kushirikiana
na Wataalamu wa Ardhi ngazi ya halmashauri husika.
Wito huo ameutoa Septemba
19,2024 wakati akitoa salamu za chama kwa Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na
Maendeleo ya Makazi Geophrey Pinda, kwenye kikao cha kusikiliza na kutatua
changamoto za ardhi kwa Wananci wa Manispaa hiyo kilichofanyika ukumbi wa
mikutano wa Ofisi ya mkuu wa mkoa wa Kilimanjaro.
Swai amesema kuendelea kuwepo kwa migogoro ya ardhi katika maeneo hayo inachangiwa sana na wananchi kununua ardhi pasipo kufuata taratibu jambo ambalo linasababisha kudidimiza shughuli za maendeleo kutokana na muda na rasilimali nyingi kutumika kushughulikia migogoro hiyo.
“Suala la migogoro ya ardhi
limekuwa kero kubwa kwa wananchi na njia pekee ya kupunguza migogoro hii ni
wananchi kurasimisha ardhi zao,”amesema Swai.
Kwa upande wake Naibu
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Grophrey, amelipongeza Baraza la
Madiwani wa Halmashauri ya Manispaa ya Moshi kwa kusimamia vema maeneo ya wazi
kutokuruhusu kuuzwa.
“Maeneo ya wazi msiweke wazo
la kuyauza, niwasihi sana Watanzania wenzangu tuendelee kuyatunza maeneo haya,”amesema
Naibu waziri Pinda.
Naye Kamishna Msaidizi wa Ardhi Mkoa wa Kilimanjaro Rehema Mdee, amesema Wizara ya ardhi Nyumba na maendelro ya Makazi imendelea kutoa huduma kwenye sekta ya ardhi kwa Watanzania, katika maeneo mbalimbali nchini ili kuhakikisha kila kipande cha ardhi kinapangwa, kupimwa na kumilikishwa.


