NA KIJA ELIAS, MOSHI.
Kuzorota kwa
uzalishaji wa kahawa katika mikoa ya kanda ya kaskazini, kumetajwa kuchagizwa
na sababu mbalimbali, ikiwemo kwa baadhi ya wakulima kubadili matumizi ya ardhi
ya kilimo kwa kujenga makazi ya kuishi.
Mkuu wa mkoa wa Kilimanjaro Nurdin Babu, ameyasema hayo Septemba 9,2024 wakati wa hafla fupi ya ufunguzi rasimi wa maandalizi ya tamasha la msimu wa Tano wa Kahawa Festival 2024, uliofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Bodi ya Kahawa nchini TCB mjini Moshi.
Amesema kubadilishwa
kwa matumizi ya ardhi ya kilimo cha kahawa kwa mikoa ya kanda ya Kaskazini kwa
ajili ya makazi na shughuli zinginezo kusababisha kushuka kwa uzalishaji wa zao
hilo.
”Watu wanabadilisha
maeneo ya kilimo cha kahawa na kujenga nyumba za makazi, nitoe wito kwa watu
wanaotaka kujenga makazi ya kuishi ni vizuri wakaenda kujenge kwenye maeneo ya
tambarare, maeneo ya mlimani ambako zao la kahawa hustawi vizuri wakayacha kwa
ajilia ya shuhughuli za kilimo cha kahawa,”amesema RC Babu.
Aidha amesema kuweko
kwa mabadiliko ya tabia nchi, mtawanyiko wa mvua, vipindi virefu vya ukame
kwenye maeneo yanayolima kahawa na matumizi duni ya pembejeo hususani mbolea za
viwandani yamesababisha pia kushuka kwa tija ya uzalishaji wa kahawa.
Amesema sababu nyingi
ambayo inasababisha kushuka kwa kiwango cha uzalishaji wa zao hilo ni pamoja na
kuyumba kwa bei ya zao kahawa duniani na hivyo kuathiri mipango ya wakulima
katika kuendeleza zao hilo.
Kwa upande wake
Mkurugenzi wa Bodi ya Kahawa Tanzania (TCB), Primus Kimaryo, amesema unywaji wa
kahawa nchini umekuwa ukisuasua licha ya utengenezaji mzuri wa kinywaji hicho.
“Tanzania tunalima
Kahawa, asilimia 93 inakwenda nje, lakini unywaji wetu bado unasuasua kwa
asilimia 7, ukipita leo mahotelini kote wanako lala wageni, licha ya Tanzania
kuwa mzalishaji mzuri sana wa kahawa, bado kahawa inayonywewa na wageni haitoi
taswira kwamba tunatengeneza kahawa nzuri kiasi hicho,” amesema Kimaryo.
Awali akizungumza Mwenyekiti
wa Kahawa Festival 2024 Denis Mahulu, amesema
ili kupata maendeleo endelevu, kuna haja ya wadau wa Kahawa kushirikiana
kwa pamoja ili kuweza kuleta maendeleo endelevu katika mnyororo mzima wa
thamani wa kahawa.
“Mnyororo unaanzia kwa
mkulima, wachakataji kuanzia ngazi ya awali, watoa huduma mbalimbali, wakiwemo
wale wa pembejeo, elimu, utafiti, wasimamizi wa zao la kahawa, pamoja na
wanunuzi wa ndani na nje ya nchi”,amesema Mahulu.
Mwenyekiti huyo
amesema namna pekee ya kuongeza unywaji wa ndani wa kahawa ni kupitia tamasha
kama hilo.
“Unywaji wa kahawa wa
ndani bado uko chini, mkakati wetu ni kupitia tamasha hili (Kahawa Fetival-2024)
litakwenda kuongeza unywaji wa kahawa kutoka asilimia 7 hadi kufikia asilimia
15,”amesema.
Aidha amesema kuwa
tamasha hilo ambalo hufanyika kila mwaka Oktoba mosi ambayo huwa ni siku ya
Kahawa duniani, na kwamba mwaka 2024 litafanyika
kwa siku tatu mfululizo ili kuhamasisha soko la ndani kwa Watanzania.
“Inatuhitaji sote
tushirikiane katika kuongeza thamani ya zao la kahawa, ili kuweza kufikia lengo
hilo ni pamoja na matamasha kama haya,” amesema Denis Mahulu, Mwenyekiti wa
Kahawa Festival 2024.
Mada mbalimbali
zitawasilishwa ikiwemo faida ya unywaji wa kahawa, kwendana na masoko ya
kahawa, matumizi ya pembejeo, matokeo yaliyofanywa na TaCRI.
Utengenezaji wa
kahawa, uonjaji wa kahawa , kushindanisha kahawa ili kuweza kupata kahawa bora
ya kahawa.
Kauli Mbiu ya Mwaka
huu; Ushirikiano wa dau kwa Pamoja katika uendelezaji wa tasnia ya Kahawa.


.jpg)