RC Babu ‘apigia debe’ushiriki wa watu Kahawa Festival-2024

MOSHI-KILIMANJARO.

Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro Nurdin Babu, amemuagiza Katibu Tawala wa Mkoa huo Kiseo Yusuf Nzowa, kuwajulisha Wakuu wa Wilaya na Wakurugenzi wa Halmashauri zote za mkoa huo, kuhakikisha kwamba wanashiriki kikamilifu kwenye Tamasha la Kahawa, litakalo kufanyika Oktoba 4 mpaka Oktoba 6 mwaka huu mkoani hapa.

Maagizo hayo aliyatoa jana wakati  wa uzinduzi wa maandalizi ya Tamasha la Msimu wa Tano wa ‘Kahawa Festival 2024’ hafla iliyofanyika ukumbi wa mikutano wa Bodi ya Kahawa  Tanzania (TCB) na kuhudhuriwa na wadau mbalimbali wa tasnia hiyo.

“Kama kweli tumeamua kuwa jambo hili, tulifanye ili liweze kuwa zuri zaidi, safari hii Katibu Tawala mkoa wa Kilimanjaro, hakikisha  Wakuu wa Wilaya na Wakurugenzi wao wote, wanashiriki katika tamasha hili, pindi tutakapoanza Kahawa Festival Oktoba 4 mwaka huu, ikiwezekana na wao wapatiwe nafasi ya kuweka mabanda yao.”amesema RC Babu.

Aidha Mkuu huyo wa Mkoa, ameitaka Bodi ya Kahawa Tanzania (TCB) na wadau wa tasnia hiyo, kuhakikisha tamasha hilo linawekwa kwenye kalenda ya serikali ya mkoa.

“Wito wangu kwa Bodi ya Kahawa na wadau wa kahawa mkoani humo, kuhakikisha sherehe za kahawa Festival, zinakuwa endelevu na ziwekwe kwenye kalenda ya serikali ya mkoa, wetu wa Kilimanjaro,”

Ameongeza kuwa kama tukio hilo litawekwa kwenye kalenda ya serikali ya mkoa, sisi tunapozungumza kwenye Kikao cha Kamati ya Ushauri ya mkoa (RCC) wajumbe watajua kwamba Kahawa Festival itakuwa ikifanyika tarehe flani hadi flani kila mwaka.

Akizungumza kuhusu uzalishaji wa Kahawa, amesema  kwa Kanda ya Kaskazini umeanza kuongezeka kwa zaidi ya asilimia 37 ukilinganisha na misimu miwili ya 2020/2022.

“Kwa mwaka 2020/2022  uzalishaji ulikuwa tani 8,811 huku misimu ya 2022/2024  uzalishaji uliongezeka na kufikia tani 14,070, ongezeko hili limeonyesha wakulima wa kahawa wa kanda hiyo kuanza kurejea kwenye kilimo cha kahawa kutokana na kuimarika kwa bei kahawa,” ameongeza.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kahawa Festival 2024 Denis Mahulu, namna pekee ya kuongeza unywaji wa ndani wa kahawa ni kupitia tamasha kama hilo.

“Unywaji wa kahawa wa ndani bado uko chini, mkakati wetu ni kupitia tamasha hili (Kahawa Fetival-2024) litakwenda kuongeza unywaji wa kahawa kutoka asilimia 7 hadi kufikia asilimia 15,ifikapo mwaka 2025,”amesema.

Kauli Mbiu ya Mwaka huu; Ushirikiano wa dau kwa Pamoja katika uendelezaji wa tasnia ya Kahawa.




Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.