MWANGA-KILIMANJARO.
Mbunge wa Jimbo la Mwanga Joseph Anania Taday o, amesema amepokea kwa huzuni kubwa taarifa za kifo cha aliyekuwa Askofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Mwanga Chediel Elinaza Sendoro.
Akiongelea kifo hicho, Mbunge Tadayo ameelezea kushtushwa kwake na kifo cha Askofu huyo ambaye amesema alikuwa ni mtu wake wa karibu, ikiwemo enzi zao wakati wakisoma wote shule ya Sekondari ya Lutheran Junior Seminary iliyoko mkoani Morogoro.
“Nimeupokea msiba huu kwa masikitiko makubwa sana kwa sababu, ukiacha tu kwamba alikuwa kiongozi wangu wa kiroho pia alikuwa rafiki ambaye tulikuwa naye wote pamoja wakati tukisoma shule ya Sekondari ya Lutheran Junior Seminary iliyoko mkoani Morogoro na baada ya kumaliza masomo yetu yeye akaenda kwenye kazi za kiroho na mimi nikaenda kusomea maswala ya Sheria,” amesema Mbunge Tadayo.
Amesema baada ya muda walikutana tena yeye akiwa Askofu wa Dayosisi ya Mwanga, huku yeye akiwa mwakilishi wa wananchi katika Jimbo hilo.
Tadayo amesema Hayati Sendoro ni mtu ambaye wamefanya nae kazi kwa karibu, huku akisema kuwa Askofu Sendoro alikuwa akipenda sana maendeleo.
“Kwa kipindi kifupi sana ambacho amekuwa madarakani Hayati Chediel Elinaza Sendoro, alifanya mambo makubwa ambayo yatakumbukwa na wana Mwanga; alikuwa na mipango mizuri sana”.
Aliendelea kusema kuwa mbali na kazi yake kama Mchungaji wa Kiroho Hayati Askofu Chediel Sendoro, pia alichukua muda wake kujishughulisha na maswala ya kimaendeleo.
“Alishiriki na kutoa mchango wake mkubwa katika shughuli za kimaendeleo ikiwemo ukanda wa tambarare ambao kuna changamoto kubwa ya ukame, ambapo alishiriki kuchimba visima virefu vya maji kwa ajili ya upatikanaji wa maji safi na salama kupitia ufadhili wa kanisa lake”, alisema.
Aliendelea kusema kuwa pia alishiriki katika kuanzisha mradi wa hoteli ya kisasa kwa ajili ya kuimarisha mapato ya dayosisi pamoja na kutoa michango mbalimbali ikiwemo ya chakula pale kinapohitajika.
Aidha Tadayo alitoa wito kwa Waumini na wananchi wote wa Jimbo la Mwanga kuwa watulivu katika kipindi hiki kigumu cha msiba huo.
Kwa mujibu wa taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa na Kamanda wa Polisi mkoa wa Kilimanjaro (SACP), ajali hiyo ilitokea eneo la Kisangiro Wilayani humo.
Alisema Askofu Sendoro alikuwa akitokea Barabara ya Njiapanda ya Himo ambako gari alilokuwa akiendesha lipata ajali ya kugongana uso kwa uso na lori na hivyo kusababisha kifo chake.
Hayati Askofu Chediel Elinaza SEndoro alizaliwa Mei Mosi, 1970 akiwa mtoto wa kwanza wa Askofu Elinaza Sendoro aliyewahi kuwa Askofu Mkuu wa KKKT Dayosisi na Mashariki na Pwani,
Baba Askofu Sendoro ameacha mjane, watoto wawili na wajukuu wawili. Askofu Chediel Sendoro alifariki dunia Septemba 9, 2024 kwa ajili ya gari wilayani Mwanga mkoani Kilimanjaro.
Askofu Chediel Elinaza Sendoro, ndiye Askofu wa Kwanza wa Dayosisi ya Mwanga, aliyeingizwa kazini Jumapili ya Novemba 6,2016, baada ya kuzaliwa kwa Dayosisi hiyo mpya iliyotokana na kugawanywa kwa Dayosisi ya Pare.

