MOSHI-KILIMANJARO.
Halmashauri ya Manispaa ya
Moshi, Mkoa wa Kilimanjaro, imetangaza majina na mipaka ya mitaa iliyoko katika
Manispaa hiyo, ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa
utakaofanyika Novemba 27 mwaka 2024.
Akitoa tangazo hilo
Septemba 16, 2024, wakati akizungumza na viongozi mbalimbali walioshiriki
katika kikao hicho kilichofanyika ukumbi wa mikutano wa halmashauri hiyo na
kuhudhuriwa na Mstahiki Meya Mhandisi Abdallah Kidumo, Mbunge wa Jimbo la Moshi Mjini, Madiwani,
Viongozi wa vyama vya Siasa, Wataalamu wa halmashauri pamoja na Watendaji wa
Kata na Mitaa.
Msimamizi wa uchaguzi huo
Mwl. Mwajuma Nasombe, ametumia fursa hiyo kuwataka Watendaji wa Mitaa kuwa
mabalozi wazuri wa kufikisha taarifa mbalimbali za uchaguzi ikiwa ni pamoja na
elimu ya uraia kwa kutoa matangazo kwa njia mbalimbali katika maeneo yao.
“Ni haki ya wananchi kupata
taarifa zote za uchaguzi kwa wakati na kwa uwazi mkubwa ili kufanya uamuzi
sahihi katika kuchagua viongozi wanaowataka, hivyo ni jukumu lenu watendaji
kuhakikisha wananchi wanapata taarifa sahihi.”amesema Mwl. Nasombe.
Msimamizi huyo wa uchaguzi, ametumia fursa hiyo kuwataka viongozi wa Serikali za Mtaa kushirikiana kwa pamoja kuweza kuwabaini
wale wote wenye sifa ambao watakuwa na haki ya kujiandikisha ili kuepusha
kuandikisha mamluki.
“Oktoba 21 mpaka 27 mwaka huu, kutakuwa na ukaguzi wa orodha ya wapiga kura, msimamizi wa uchaguzi ana wajibu wa kubandika orodha ya wapiga kura ili kutoa fursa kwa wananchi waliojiandikisha kuhakiki majina yao ili kupata fursa ya kutumia haki yao ya kimokrasia,”amesema Mwl. Nasomnbe.
“Novemba Mosi hadi Novemba 7
mwaka huu litakuwa ni zoezi la kuchukua na kurudisha fomu za kugombea, hivyo
niwaombe Watanzania wote wenye sifa za kugombea wajitokeza kwa wingi ili kuweza
kupata fursa ya kugombea pale ambapo watakuwa wamekidhi vigezo.
Amesema Novemba 1 hadi 7 itakuwa
ni siku ya kuchukua fomu na kuirejesha
na Novemba 8 itafiuata ratiba ya uteuzi ya wagombea na baada ya hapo Novemba
20 mpaka novemba 26 mwaka 2024 wale wote ambao watakuwa wamepewa dhamana na
kuteuliwa wanahaki ya kufanya kampeni na Novemba 27 itakuwa ni siku ya kufanya
uchaguzi.
Vile vile amesema kuwa Novemba
11 mpaka 20 mwaka huu itakuwa siku ya wananchi kujitokeza kujiandikisha kwenye
daftari la mkazi, huku akisema kuwa ni wajibu watendaji hao kuwakumbusha
wananchi mwenye sifa za kujiandikisha waweze kujitokeza kujiandikisha.
“Mwananchi mwenye sifa za
kujiandikisha kwenye daftari la mkani ni yule ambaye atakuwa na sifa nne kwa
anatakiwa kuwa raia wa Tanzania, awe na
akili timamu, awe mwenye na umri kuanzia miaka 18, lakini pia lazima awe mkazi wa mtaa husika.”amefafanua.
Aidha ametumia fursa hiyo
kuwataka viongozi wote wa Serikali za Mtaa walioko madarakani ifikapo Oktoba 25
mwaka huu, watakuwa na wajibu wa kuzirudisha nyaraka zote za Serikali ambazo walikabidhiwa kwa sababu uongozi wao
utakuwa umefika ukomo.
Uchaguzi wa Serikali za
Mitaa hufanyika kila baada ya miaka mitano, kwa kuzingatia matakwa ya Sheria ya
Serikali za Mitaa, Mamlaka za Mitaa sura 287 na Sheria za Mitaa ya Mamlaka za Mji
sura 28, ambapo wananchi hutumia haki yao ya kikatiba kuomba kuongoza wenzao na
kuchagua viongozi katika maeneo wanayoishi.
Uchaguzi utakaofanyika Novemba
27 mwaka 2024, utakuwa ni wa saba tangu mfumo wa vyama vingi vya siasa kuingia nchini
mwaka 1992.











