Balozi wa Tanzania
nchini Japan Baraka Luvanda, Osamu
Aizawa, Meneja Mkuu wa Kampuni ya ITO EN na Wawakilishi wa Kampuni ya
Tully’s Coffee, Wakiwa katika picha ya pamoja kwenye hafla ya uzinduzi wa Kahawa ya Tanzania iliyofanyika jijini Tokyo, Japan.
TOKYO-JAPAN
Kampuni ya ITO EN LTD, ambayo ni kampuni tanzu ya Tully’s Co. Ltd., inayomiliki migahawa maarufu ya Tully’s Coffee, imezindua aina tatu mpya za kahawa ya Tanzania, nchini Japan katika hafla iliyofayika jijini Tokyo tarehe 14 Machi, 2024.
Aina za kinywaji hicho pendwa nchini humo kinachotokana na kahawa kutoka Tanzania ni Tully’s Coffee Barista Black Kilimanjaro; Tully’s Coffee my home black Kilimanjaro; na Tully’s Coffee Barista roast old brew –Kilimanjaro blend.
Kahawa hizo ni kutoka mkoa wa Arusha, Tarime mkoani mara na mashamba ya GDM yaliyoko Mbozi mkoani Mbeya.
Zoezi hilo la uzinduzi lililofanyika katika Ubalozi wa Tanzania Jijini Tokyo na liliongozwa na Balozi wa Tanzania nchini Japan Baraka Luvanda, lilimshirikisha pia Meneja Mkuu wa Kampuni ya ITO Osamu Aizawa, aliyeambatana na wawakilishi wa kampuni hiyo na Kampuni ya Tully’s Coffee.
Kampuni ya ITO EN Ltd. ambayo, ni kampuni tanzu ya Tully’s Coffee ni kampuni inayoongoza kwa biashara ya vinywaji nchini Japan, inamiliki migahawa ya kahawa takriban 700 nchini humo huku ikiwa imejipatia umaarufu mkubwa katika biashara ya uuzaji wa kahawa aina mbalimbali duniani.
Ni mara ya pili, kwa Kampuni ya Tully’s kuzindua kahawa ya Tanzania katika migahawa yake, uzinduzi kama huu uliwahi kufanyika mwezi Juni na Agosti 2023 ukihusisha kahawa aina ya GDM full washed, GDM natural na Tarime Coffee.
Kuzinduliwa kwa aina nyingine tatu mpya za kahawa nchini Japan, kunaendelea kuleta uhakika na kuongezeka kwa soko la kahawa ya Tanzania nchini Japan ambayo imejizolea umaarufu mkubwa kwa ubora na ladha ya aina yake na kupelekea kupewa jina maarufu la kibiashara la Kilimanjaro Coffee.
Kilimanjrao Coffee ni miongoni mwa bidhaa tatu za kahawa zinazopendwa zaidi Japan; na jina hilo hutumika nchini humo kwa kahawa zinazozalishwa Tanzania pekee, kwa kutambua kivutio kikubwa cha Mlima Kilimanjaro uliopo nchini Tanzania.
Tanzania inasifika Japan kwa kuzalisha kahawa bora aina ya Arabica (Arabica laini-full washed na Arabica ngumu-natural) inayolimwa katika mikoa ya Kilimanjaro, Arusha, Manyara, Mara, Tanga, Morogoro, Njombe, Iringa, Katavi, Rukwa, Ruvuma, Kigoma, Songwe na Mbeya; na kahawa ya Robusta inayolimwa mkoani Kagera.
Akizungumza katika uzinduzi huo, Balozi Baraka Luvanda alizihakikishia kampuni za Japan, uwepo wa mazingira wezeshi ya biashara na uwekezaji wanapoamua kuwekeza katika kilimo au sekta nyinginezo hapa nchini.
Balozi Luvanda amelitaja zao la kahawa kuwa ni miongoni mwa mazao ya kimkakati yanayongoza kwa kulipatia Taifa pato na kuingiza fedha za kigeni.
Aidha, Balozi Luvanda alielezea
juhudi za Serikali ya Awamu ya Sita, inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan, kuwa imefanya mageuzi
makubwa katika sekta ya kilimo kwa kuwekeza katika miradi ya muda mrefu na
mfupi ikiwemo kutatua changamoto za kilimo kuanzia shambani hadi sokoni ili
kujihakikishia uhakika wa chakula na biashara.






