Ded Nasombe: Wananchi jitokezeni kushiriki Uchaguzi Serikali za Mitaa

MOSHI-KILIMANJARO

Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya Manispaa ya Moshi Mwl. Mwajuma Nasombe, amewataka wakazi wa Manispaa hiyo, kujitokeza kwa wingi kushiriki uchaguzi wa Serikali za Mitaa unaotarajia kufanyika Novemba 27, 2024.

Wito huo umetolewa jana Septemba 28,2024 wakati akizungumza na wakazi wa Manispaa hiyo waliojitokeza kuangalia bonanza kati ya timu ya Umoja wa Bajaj na Bodaboda waliocheza na timu ya Watumishi wa Manispaa hiyo, bonanza lililokuwa limelenga kuhamasisha Uchaguzi wa Serikali za Mitaa 2024 lililoandaliwa na Manispaa hiyo.

Nasombe amesema kuwa ili mwananchi aweze kupiga kura siku ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa, anapaswa kujiandikisha katika Daftari la Kudumu la mpiga kura, ambapo zoezi la uandikishaji litafanyika kuanzia Octoba 11 hadi 20, 2024.

“Mwaka huu tutakuwa na zoezi kubwa la Uchaguzi wa Serikali za Mitaa, utakaofanyika Novemba 27,2024, niwaombe Wakazi wa Manispaa ya Moshi, tujitokeze kwa wingi wetu tushiriki uchaguzi huu kwa Maendeleo ya Kata zetu, usikubali mtu mwingine akuchagulie kiongozi wakati una uwezo wa kupiga kura,” amesema Mwl. Nsombe.

Kwa upande wake Katibu Tawala Mkoa wa Kilimanjaro Kiseo Yusuf Nzowa, ametoa wito kwa wananchi wote wa mkoa huo, kujitokeza kushiriki uchaguzi huo wa Serikali za Mitaa.

“Nikupongeze sana Mkurugenzi Mwajuma Nasombe kwa ubunifu wako huu na kuweza kuandaa bonanza hili la michezo mbalimbali kama sehemu ya hamasa kuelekea Uchaguzi wa Serikali za Mitaa ambao utafanyika Novemba 27, 2024,”amesema Nzowa.

Akizungumza Msimamizi msaidizi wa uchaguzi Manispaa ya Moshi Denis Robert Shette, amesema kabla ya kuanza kwa bonanza hilo, halmashauri ya Manispaa ya Moshi iliandaa maandamano ambayo yalianzia katika ofisi za Manispaa, kupitia Stendi kuu ya mabasi hadi katika Uwanja wa mpira Majengo, ambako bonanza hilo lilipofanyikia.

Amesema bonanza hilo, lilihusisha mpira wa wavu, kwa timu ya Wanawake kutoka Chuo Kikuu cha Ushirika Moshi (MoCU) ambayo ilicheza na timu ya Wanawake ya Manispaa ya Moshi.
Shette amesema michezo mingine iliyofanyika katika uwanja huo ni pamoja na mashindano ya kunywa soda na mchezo wa ngumi uliohusisha mabondia kutoka Chama cha Ngumi Mkoani Kilimanjaro.









Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.