Wanaume watakiwa kuvunja ukimya, taarifa vitendo vya ukatili

Wanaume wametakiwa kuvunja ukimya na kutoa taarifa za vitendo vya kikatili ambavyo wamekuwa wakifanyiwa na wake zao manyumbani ikiwemo vipigo na kinyimwa unyumba, ili hatua ziweze kuchukuliwa mapema  kabla ya madhara kuwa makubwa.

 

Wito huo umetolewa na Sajent Mwajabu Mzee, kutoka Dawati la Jinsia na Watoto Mkoa wa Kilimanjaro, wakati akizungumza kwenye Baraza la  Vijana  wa Moshi Vijijini, lililofanyika katika Hifadhi ya Msitu wa Rau, Mkoani humo.

 

Sajent Mwajabu amesema, kumekuwepo na vitendo vingi vya kikatili katika jamii kwa sasa lakini wanaume wengi na hata vijana wamekuwa na hofu ya kutoa taarifa, jambo ambalo limekuwa likiwafanya kuumia na hata wengine kuchukua maamuzi magumu ya kujiua.

 

Aidha amewaonya vijana kuacha tabia ya kujipiga picha za utupu na kitumiana kwenye mitandao ya kijamii kwa kuwa picha hizo zinaweza kutumiwa vibaya na kupelekea watu kuathirika kisaikolojia na hata kusababisha vifo.

 

Vilevile amewataka vijana kusaidia kuibua vitendo vya kikatili vinavyofanyika katika jamii, ili hatua za kisheria ziweze kuchukuliwa dhidi ya wahusika.

 

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa Chama cha Mapinduzi (UVCCM) Wilaya ya Moshi Vijijini, Yuvenal Shirima, amewataka vijana kuwa mfano wa kuigwa katika jamii na kuepuka kujihusisha na vitendo vya kikatili.

 

Akizungumza mmoja wa vijana waliohudhuria baraza hilo Rose James, amesema ukatika katika jamii umeendelea kushika kasi kila kukicha na kwamba zinahitajika jitihada za pamoja za wanajamii katika kukabiliana na vitendo hivyo.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.