Chama cha Ushirika Mweka Sungu chapata Mil. 250

CHAMA cha Ushirika wa Mazao na Masoko cha Kibosho Mweka Sungu, kimepata ruzuku yenye thamani ya shilingi milioni 250 kwa ajili ya kuboresha Kilimo cha Kahawa inayozalishwa na chama hicho.

Akiongea wakati wa uzinduzi wa mradi wa maboresho ya kahawa utakaotekelezwa kupitia ruzuku hiyo, Mwenyekiti wa Kibosho Mweka Sungu Amcos Medard Mrema, amesema kuwa kupitia mradi huo uzalishaji wa kahawa unatarajiwa kuongezeka na hivyo kuboresha maisha ya Wakulima na kuimarisha uchumi wa wilaya, Mkoa na hata Taifa kupitia zao la kahawa.

Aidha ameishukuru Taasisi ya Maendeleo ya Afrika ya Marekani USADF kwa kukubali maombi ya chama hicho ya ruzuku ambapo amesema kukubaliwa huko kutaongeza uzalishaji wa, mapato ya chama na mtu mmoja mmoja pamoja na kuongeza fedha zitakazotumika kuchangia maswala ya maendeleo.

Akizungumzia uzalishaji wa zao la kahawa Mwenyekiti huyo amesema uzalishaji wa kahawa  umeshuka kutoka kilo 18,160 msimu wa 2021/2022 hadi kufikia kilo 10,568 msimu wa 2023/2024; na kwamba mradi huo umekuja muda muafaka wakati wakiendelea na mipango inayolenga kuongeza uzalishaji wa zao hilo.

Amesema tangu mwaka wa 2005 hadi sasa chama hicho kimeshafadhili wanafunzi 120 kupata elimu katika ngazi mbalimbali; ambapo pia kimeweza kuchangia katika ujenzi wa zahanati ya Mweka,  shule ya sekondari za Cyril Chami na Sungu, pamoja na kuchangia miundombinu mingine ya elimu kama vile madawati.

Kwa upande wake Mratibu mkazi wa Mradi wa USADF Nchini Tanzania Gilliard Nkini, amesema taasisi hiyo ya Marekani inashirikiana na ya Serikali ya Tanzania katika kuboresha Sekta ya Kilimo nchini ikiwemo kwenye eneo la kilimo.

Amesema USADF  wako kwenye nchi 22 za Afrika na katika nchi zote hizo kazi kubwa ni kushirikiana na serikali za nchi hizo katika kukuza maendeleo kupitia wakulima wadogo wadogo.

Akizungumzia mkataba ambao wamesainia na chama hicho Nkini amesema kupitia mradi huo USADF imekipatia chama cha ushirika Kibosho Mweka Sungu kiasi cha SH milioni 250  fedha ambazp zitakwenda kutumika katika kuboresha upatikanaji wa pembejeo za kilimo ambazo ni muhimu katika uzalishaji wa kahawa, ambapo wakulima watazipata kwa ukaribu zaidi maeneo yao badala ya kuifuata mbali.

Naye Eileen Mwakisese kutoka ADC Tanzania ambao ndiyo watasimamia mradi huo, amesema mradi huo unatarajiwa kuongeza uwezo wa Chama cha Kibosho Mweka Sungu katika usimamizi wa fedha ili kupata maendeleo endelevu na pia kuandaa mpango biashara, ambao ndio utatumika kama dira ya chama.

Akizungumza Mrajis Msaidizi wa Ushirika mkoani Kilimanjaro, Jackline Senzighe, ametoa wito kwa uongozi wa Chama cha Kibosho Mweka Sungu, kuhakikisha wanatumia vyema ruzuku hiyo ili kuongeza tija katika uzalishaji wa kahawa na hivyo kuongeza mapato na kuboresha maisha ya wanachama wake. 









Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.