TRA yaendesha mafunzo washauri wa kodi Kilimanjaro

Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imeendesha mafunzo ya siku moja kwa Washauri wa kodi mkoani  Kilimanjaro kuhusu mabadiliko ya sheria mpya za kodi.

Mafunzo hayo yalifanyika jana katika ukumbi mdogo wa Hazina ndogo iliyoko mkoani humo lengo likiwa ni kuwapa uelewa wafanyabiashara  kutambua mabadiliko ya sheria hizo zilizoanza kutumika Julai mwaka huu .

Akizungumza Ofisa Msimamizi wa Kodi TRA kutoka Makao Makuu,  Alexs Mwambeja, alisema kwenye mabadiliko hayo ya sheria mpya za kodi kuna vipengele ambavyo viwango vya kodi vimeshushwa na vingine vimeongezwa.

Alisema Serikali imeweka malengo ya kukusanya mapato ya Sh Trilioni 49.35 ambapo TRA imepangiwa kukusanya kiasi cha Sh Trilioni 30.4 sawa na asilimia 62 ya makusanyo yote ya mapato ya Serikali.

Amesema kiasi cha Sh Trilioni 30.4 ni ongezeko la Trilioni 2.1 ukilinganisha na kiwango walichopangiwa mwaka 2023/2024. cha kukusanya Trilioni 28.3.

“Lengo hilo limewekwa kutokana na kuweko kwa viwango vipya vya mapato ikiwemo ukusanyaji wa kodi katika watengeneza waudhui, pamoja na wauzaji wa mali za kidigital hivyo ni lazima mapato hayo yatoke kwenye vyanzo mbalimbali vya mapato na walipa kodi wanatakiwa kutambua sheria ya mabadiliko hayo ya kodi.”alisema.

Amesema kwa bajeti hiyo TRA ina uhakika inaweza kutimiza lengo la kukusanya Sh Trilioni 30.4 ili kuweza kufikisha ndoto za Rais Samia Suluhu Hassan, katika kupeleka huduma bora kwa jamii.

Kwa upande wake Ofisa Msimamizi wa Kodi Mwandamizi Mkoa wa Kilimanjaro na Mkuu wa Kitengo cha Elimu na Mawasiliano Oldupai Papaa, amesema katika mabadiliko hayo ya sheria mpya ya kodi kwa mwaka wa fedha 2024/2025 eneo moja wapo ambalo sheria hiyo imeweza kuongeza mapato ni kwenye viwanywaji ambavyo havikuchakatwa ikiwemo Chibuku.

“Chimbuku imeweza kuongezewa kodi ya ushuru wa bidhaa kwa Sh 900 kwa lita moja na mkoa wetu wa Kilimanjaro una maeneo mengi  ambayo yanazalisha vinywaji vya namna hiyo.

Aidha amesema kuwa vinywaji vingi vimekuwa vikitengenezwa majumbani kama TRA Mkoa wa huo wameweka mkakati wa kuhakikisha vinywaji vyote vitakavyotengenezwa na kuwekwa kwenye pakiti na kwenda kuuzwa vitatozwa kodi.

Pia alisema TRA Mkoa wa Kilimanjaro imetenga siku maalum ya kusikiliza changamoto kutoka kwa wafanyabiashara ambapo kila siku ya Alhamisi watakuwa wakisikiliza changamoto hizo.

“Mfanyabiashara yeyote mwenye changamoto yake, atatakiwa kufikia kwenye Ofisi zetu za TRA kila siku ya Alhamisi ambapo Meneja pamoja na Wataalam wengine watakuwepo kusikiliza changamoto zao,”alisema.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.