Takukuru yaanza uchunguzi hongo kuelekea uchaguzi Serikali za Mitaa

Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Kilimanjaro (PCCB), imeanza uchunguzi kwa watu ambao wanadaiwa kuwania nafasi mbalimbali za uongozi, kuanza kutoa hongo kwa kuwanunulia wananchi vitu mbalimbali kama vile sukari, nyama choma, pombe aina ya mbege, ili kuwashawishi kuwachagua katika uchaguzi ujao.

Inadaiwa kuwa watu hao wameanza kugawa chumvi, vitenge huku wengine wamediriki kuwapikia (Pilau) kwa lengo tu kwamba kitakapopul;izwa kipyenga cha uchaguzi wawapigie kura.

Akizungumza katika semina ya siku moja mjini Moshi, Mkuu wa Takukuru mkoa wa Kilimanjro Musa Chaulo, alisema wamepata taarifa zisizo na mashaka watu kulishwa pilau, kuchinja ng’ombe na kuwagawia nyama, kuwanywesha pombe aina ya mbege, nyama choma kuwapa sukari na vitenge huku dhima nzima za matukio hayo sio kusaidia bali ni kuendeleza ushawishi kuelekea uchaguzi wa Serikali za Mitaa 2024 na Uchaguzi Mkuu wa 2025.

“Wanasiasa wanapotaka kuingia madarakani, wanatumia matendo mengine ambayo sio sahihi ambayo kwetu sisi tunayatafsiri kwamba ni vitendo vya rushwa pale wanapotoa mali, wanapotoa pesa au zawadi, tunazo taarifa wengine wameanza  kuchinja ng’ombe na kuwagawia nyama, wengine wameanza kuwanywesha watu pombe aina ya mbege,  kutoa sukari na kuongeza kuwa;

Wengine wanagawa chumvi, vitenge, kuwapikia pilau ili kushawishi watu ikifika wakati wa uchaguzi wawapigie kura hivi vyote tunavitafsiri kama vitendo vya rushwa, unapojihusisha na vitendo vya rushwa unakuwa umetenda kosa la jinai.”

Alisema Waandishi wa Habari ni wadau muhimu katika vita ya kutokomeza rushwa hivyo wanawajibu mkubwa wa kuhakikisha wanasaidia kuzuia vitendo vya rushwa katika jamii.

“Ili tuweze kupambana na rushwa nchini, sisi kama TAKUKURU hatuwezi kusimama sisi wenyewe kupambana dhidi ya vitendo vya rushwa ni sharti la kisheria linalotutaka kuwashirikisha waandishi wa habari,”alisema.

Alisema “Kifungu cha 7 (b) kikisomwa pamoja na kifungu cha 45 cha sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa sura ya 329 kinatambua umuhimu wa vyombo vya habari katika mapambano dhidi ya rushwa,”alisema Chaulo.

Kwa upande wake Mwanasheria wa Takukuru Mkoa wa Kilimanjaro Samweli Gabriel alisema tafsiri rasimi ya rushwa ni mtambuka na kwamba wao wapo kuthibitisha matendo yanayotafsiriwa kama ni rushwa na kutoa ushahidi usio na shaka.

Akizungumza mmoja wa Waandishi wa habari kutoka kituo cha Star TV Rodrick Mushi, aliishukuru TAKUKURU kwa kuweza kutoa Semina hiyo kwa Waandishi wa habari, ambapo alisema semina hiyo imewajengea uwezo zaidi katika kuongeza kasi ya kupambana na vitendo vya rushwa katika chaguzi zijazo.

Naye Mwenyekiti wa Chama cha Waandishi wa habari Mkoa wa Kilimanjaro (MECKI) Bahati Nyakiraria, aaliwataka waandishi wa habari kufuata maadili na misingi ya uandishi wa habari ili kuandika habari pasipo kuegemea upande mmoja.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.