Sekondari ya Asha-Rose Migiro jenga madarasa mengine inayogharimu Mil. 429

MWANGA, KILIMANJARO

Changamoto ya uhaba wa madarasa kwa kidato cha tano na sita katika shule ya Sekondari Dkt. Asharose Migiro, iliyoko Halmashauri ya Wilaya ya Mwanga, mkoani Kilimanjaro inakwenda kuwa hisitoria baada ya  serikali kujenga miundombinu ya madarasa katika shule hiyo.

Utatuzi wa changamoto hiyo, unatokana na Serikali Kuu kutoa kiasi  cha Sh milioni 429, kwa ajili ya kutekeleza mradi wa ujenzi wa madarasa sita na ofisi tatu, mabweni mawili na choo matundu kumi, kwa ajili ya kupanua shule hiyo kuwa na kidato cha tano na sita.

Mkuu wa shule ya Sekondari ya Dkt. Asharose Migiro Bi. Flaviana Sumawe, ameyasema hayo Julai 27,2024, wakati akisoma taarifa ya mradi wa ujenzi huo kwa Mbunge wa Jimbo la Mwanga Joseph Tadayo, aliyetembelea shule hiyo kwa ajili ya kujionea shughuli za maendeleo zinazoendelea shuleni hapo sambamba na kuweka jiwe la msingi katika vyumba vya madarasa hayo.

Amesema shule ya Sekondari Dkt. Asharose Migiro, ilifanikiwa kupata fedha kutoka Serikali Kuu jumla ya Sh milioni 429 kwa ajili ya kutekeleza mradi wa ujenzi wa mabweni mawili, madarasa sita na ofisi tatu na choo matundu kumi kwa ajili ya kupanua shule kuwa na kidato cha tano na sita.

Amesema  kukamilika kwa mradi huo, unakwenda kuiwezesha shule ya Dkt. Asharose Migiro, kutoa mazingira mazuri ya kufundishia na kujifunzia ambapo unawezesha watoto wa kike wa Kitanzania kutimiza ndoto zao.

“Kwa niaba ya Jumuiya ya shule napenda kutoa shukrani za dhati kwa Serikali ya awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuipatia shule yetu fedha za kutekeleza mradi huu, mkubwa ambao unaipandisha shule hadhi na kuwa na kidato cha tano na sita.”amesema Mwl. Sumawe.

Aidha Mkuu huyo wa shule, alimshukuru Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mwanga kwa ushirikiano anaoupata kupitia Idara ya Elimu Sekondari na Idara ya Uhandisi wa Majengo.

Kwa upande wake Mkurugenzi mtendaji  Halmashauri ya Mwanga Zahara Msangi, amemshukuru Rais Samia kwa kazi kubwa ambayo, ameendelea kuifanya katika halmashauri hiyo kwa kuiletea fedha nyingi za miradi ya maendeleo.

Amesema  Shule ya Sekondari ya  Dkt. Asharose Migiro, imekuwa shule ya mfano katika matokeo ya kidato cha nne kwa zaidi ya miaka mitano iliyopita, jambo ambalo limeisukumua serikali kuona umuhimu wa kuiongezea madarasa kwa ajili ya kidato cha tano na sita na kuiwezesha halmashauri hiyo  kuongeza idadi ya sule za kidato cha sita, kutoka shule sita zilizopo na kufikia idadi ya shule nane.

Akizungumza Mbunge wa Jimbo la Mwanga Joseph Tadayo, amesema shule ya Asharose Migiro ni moja kati ya shule bora hapa Tanzania ambazo zinafanya vizuri kitaaluma, huku kipongeza miundombinu iliyojengwa kiwango cha kuridhisha.

Pia,  Mbunge Tadayo ameishukuru serikali ya awamu ya sita ikiongozwa na Rais Samia Suluhu Hasani kwa kuleta fedha nyingi za miradi ya maendeleo kwa wananchi ndani ya jimbo hilo.

Akitoa neno la shukrani kwa niaba ya wanafunzi wenzake, mmoja wa wanafunzi hao, ameishukuru serikali kwa kuwezesha kujenga miundombinu ya madarasa katika shule hiyo.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.