TRITA yatoa Mafunzo Uhamiaji na Utaratibu wa Uhamiaji

Chuo cha Kikanda cha Uhamiaji (TRITA) Kilichopo Wilaya ya Moshi Mkoani Kilimanjaro, kimetoa mafunzo ya uhamiaji na utaratibu wa uhamiaji (Essentials of Migration training) kwa taasisi za kiserikali na binafsi zaidi ya 300 tangu kuanzishwa kwake mwaka 2007.

Kamishna Jenerali wa Uhamiaji nchini (CGI), Dkt. Anna Makakala, aliyasema hayo jana, wakati akifungua semina ya mafunzo ya uhamiaji na utaratibu wa uhamiaji yanayofanyika Chuoni hapo ambapo takribani washiriki zaidi ya 30 wa mafunzo hayo wamehudhuria mafunzo hayo ya siku tano ambapo yatahitimishwa Agosti 23 mwaka huu.

Akifungua mafunzo hayo kwa niaba ya Kamishna Jenerali wa Uhamiaji nchini, Kamishina wa Mafunzo na Maendeleo wa uhamiaji Amiru Sadiki alisema mafunzo hayo yamelenga kutoa mafunzo ya kuwajengea na kukuza uwezo wa kiutendaji Watumishi wa Jeshi la Uhamiaji na wadau wengine wa maswala ya uhamiaji Kitaifa na Kimataifa ili kukabiliana na wimbi la wahamiaji haramu hapa nchini.

Kamishina Sadiki aliendelea kusema kuwa mafunzo hayo ni sehemeu ya utekelezaji wa matakwa ya uanzishwaji wa Chuo cha TRITA lengo likiwa ni kuimarisha usalama wa nchi.

Alisema mafunzo hayo yamenga kuimarisha utoaji wa huduma zinazohusiana na maswala ya uhamiaji ikiwemo jinsi ya kufanya maombi bila makosa kwa wale wanaohitaji huduma zinazohusiana na maswala ya uhamiaji.

Akizungumzia kuhusu mafanikio yaliyokwisha kupatikana tangu kuanzishwa kwa Chuo hicho, Kamishina Sadiki alisema ni pamoja na watumishi na wadu wengine kupata uelewa utakaowawezesha kukabiliana na changamoto ya wageni wasio na vibali stahiki na wale waio na vibali kabisa (compliance).

Akiongelea mafuzo hayo Mkuu wa Chuo cha Kikanda cha Uhamiaji (TRITA) Kamishna Msaidizi wa Uhamiaji Hoja Mahiba, alisema kuwa tangu kuanzishwa kwa chuo hicho 2007 chuo kililenga kutoa mafunzo kwa maofisa wa Uhamiaji Kikanda.

Alisema kadiri mahitaji yanayohusiana na maswala ya uhamiaji yalivyozidi kuongezeka, waliamua kutanua wigo wa mafunzo ambapo kwa sasa yanawashirikisha wadau wengine zikiwemo taasisi binafsi katika kutekeleza majukumu yanayohusiana na masuala ya uhamiaji.

Alisema mafunzo hayo ni ya awamu ya 23 tangu kuanzishwa kwake mwaka wa 2019 na moja wapo ya mafanikio ya mafunzo haya ni pamoja na kuimarika kwa ushirikiano kati ya Jeshi la Uhamiaji na wadau wengine katika upatikanaji wa taarifa zinazohusiana na taarifa za wageni wanaoingia na kutoka hapa nchini.

Kwa upande wao baadhi ya washiriki wa mafunzo hayo Goda Jeremiah na Mohamed Omari, walisema kuwa wanatarajia kupata elimu itakayomwezesha kupata uelewa wa ziada katika kuhudumia wawekezaji na wageni wanaoingia hapa nchini.








Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.