HIMO, MOSHI VIJIJINI
Wananchi wa kitongoji cha Kisimani na Msufini vilivyopo katika Mji mdogo wa Himo, Halmashauri ya Wilaya ya Moshi Vijijini wameishukuru serikali kupitia wakala wa Barabara za Vijijini na Mjini (Tarura) kuwajengea daraja la kudumu linalounganisha nchi mbili ya Tanzania na Kenya, ambapo wamesema kuwa kukamilika kwa daraja hilo jipya litasaidia kuepusha maafa.Wananchi hao wametoa shukrani hizo Agosti 18, 2024 mbele Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi Taifa Abudul Fadhil Rajabu, alipotembelea na kukagua maendeleo ya ujenzi wa daraja hilo lililopo Kata ya Makuyuni katika mji mdogo wa himo, ambapo Serikali imetoa kiasi cha zaidi ya Sh milioni 423.1.
Mkazi wa Kijiji cha Makuyuni Florah Sindibaki, amesema alishindwa kuvuka katika moto huyo kwa ajili ya kwenda kujitafutia kutokana na korongo hilo kuwa refu jambo ambalo lilimsababishia kukaa ndani kwa kipindi kirefu.
Naye Paulo Mlaki, amesema kujengwa kwa daraja hilo limewasaidia wananchi wa maeneo hayo kusukuma maendeleo yao na kumaliza usumbufu wa muda kwa kuvuka kwenye maji kila wanapotaka kusafiri kwenda maeneo mengine ikiwemo makao makuu ya wilaya kwa ajili ya kufuata huduma mbalimbali za kijamii.
Mkazi mwingine wa Makuyuni Samwel Mlay, amesema kutokana na korongo hilo kuwa kuwa wamama wajawazito walikuwa hawawezi kuvuka kwa ajili ya kwenda kujifungua hospitalini na kulazimika kujifungulia nyumbani, huku wananchi wengine walilazimika kuzunguka hadi umbali wa kilometa sita ambako ni umbali mrefu, hivyo kuwapotezea muda mwingi ambao wangeweza kutumia katika shughuli za maendeleo.
Akizungumza Mtendaji wa Kata ya Makuyuni Jafari Juma Mbwambo, amesema wakati wa masiki watoto walikuwa hawawezi kuvuka kwenda shule kwa kuhifia kusombwa na maji, kukamilika kwa daraja hilo shughuli za usafiri na usafishaji wa mazao zinakwenda vizuri tofauti na zamani na kuipongeza Serikali kupitia amewapongeza TARURA kwa ujenzi wa mradi huo wa daraja.
Aidha amesema kukamilika kwa daraja hilo mbali na kupunguza adha waliyokuwa wakiipata wananchi hao, pia litakwenda kufungua fursa za kiuchumi kati ya nchi hizo mbili Tanzania na Kenya.
Akisoma taarifa fupi ya ujenzi wa daraja hilo Meneja wa Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) Wilaya ya Moshi Mhandisi Africano Orota, amesema ujenzi wa daraja hilo utaongeza usalama wa watumiaji wa barabara kwenda kujipatia hufduma mbalimbali za kijamii , shughuli za kilimo na wanafunzi kwenda kupata elimu kutoka upande mmoja kwenda mwingine.
Amesema ujenzi wa daraja hilo ulianza mwezi Mei mwaka huu na unatarajiwa kukamilia Novemba 2024, huku akisema kuwa kabla ya ujenzi wa daraja hilo, kulikuwa na daraja la muda lililojengwa na Diwani wa Kata hiyo Dixson Tarimo, ambalo lilikuwa sio salama kwa watumiaji.
Kwa upande wake Diwani wa Kata hiyo Dixson Tarimo, amesema takribani miaka 20 wakazi wa vitongoji walilazimika kuzunguma umbali wa kilometa 6 lakini kukamilika kwa daraja hilo watatumia umbali wa kilometa moja kuweza kufika mji mdogo wa Himo kwa ajili ya kujitafutia.
Aidha amesema kwa kipindi cha miaka mine ya Serikali ya wamu ya sita Kata hiyo imeletewa fedha zaidi ya Sh bilioni 2 kwa ajili ya shughuli za maendeleo.