Zaidi ya wanariadha 1,000 kutoka ndani na nje ya mipaka ya Tanzania Agosti 25,2024 walishiriki katika mashindano ya mbalimbali yakiwemo mashindano ya kuendesha baiskeli km 75, mbio ndefu za Km 21, mbio fupi za km 5 matembezi ya msituni kwa kutembea peku peku, ikiwa ni kilele cha cha msimu wa Pili wa Tamasha kubwa la Tukacharu Rau Forest mtoko Nyikani ambalo lilifanyika katikati yam situ huo uliopo Wilaya ya Moshi mkoani Kilimanjaro.
Akizungumza jana Agosti 25,2024 mara baada ya kumaliza mbio za kilometa tano mshindi wa kwanza Esaya Isaack, amesema mbio hizo zimekuwa za kipekee tofauti na mbio ambazo wamekuwa wakikimbia kuwa katikati ya miji na majiji ambao huo kuwa msongamano wa watu na magari.
Isaack amesema utaratibu uliofanyika wa mbio za Tukacharu Rau Forest Season 11 2024 za kukimbia ndani ya hifadhi ya Rau Forest ni moja ya kuvitangaza vivutio vya utalii vilivyomo ndani ya hifadhi hiyo.
Naye mshindi wa pili katika mbio hizo Kelvine Sarakikya, ameushauru uongozi wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS )Wilaya ya Moshi mkoani Kilimanjaro, kutengeneza mabango mengi zaidi, ambayo yatakuwa yakionesha njia za kupita pamoja na kuziboresha njia za wanariadha kukimbia sambamba na kuongeza motisha kwa washiriki wa mbio hizo hali ambayo itaongeza idadi ya washiriki wengi zaidi
Amesema ukimbiaji ndani ya hifadhi ni mzuri zaidi tofauti na mbio ambazo hufanyika barabarani ambapo wakimbiaji wengi huhofia kukanyagwa na magari
Awali akizungumza Ofisa Misitu Daraja la Pili (TFS) Wilaya ya Moshi Zayana Mrisho Hashim, amesema mashindano hayo ni moja kampeni zinazohamasisha masuala ya uhifadhi wa misitu, ambapo tangu kuasisiwa kwake mwaka 2023 washiriki wa mbio hizo wamezidi kuongezeka.
Naye Afisa Utalii TFS katika Hifadhi ya Msitu Rau Aljabir Nurdin Semkiwa, amesema watu wengi walioshiriki mbio hizoza Tukacharu Rau Forest Season 11, wengi walivutiwa na utalii wa kutembea pekupeku ambapo idadi kubwa ya watu walijitokeza kushiki matembezi hayo akiwemo Mkuu wa Wilaya ya Mwanga Abdallah Mwaipaya.
Amesema hifadhi ya Msitu wa Rau ni hifadhi ya pekee ambapo mtalii akifika ndani ya hifadhi hiyo anaweza kufanya utalii wa matembezi ya pekupeku tofauti na hifadhi zingine zilizopo hapa nchini.