Machifu Kilimanjaro wampongeza Rais Samia kuwa mwenyekiti wa SADC

Umoja wa Machifu Mkoa wa Kilimanjaro na Baraza la Wazee la Ushauri la Kiserikali mkoani humo, wamempongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuchaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Siasa, Ulinzi na Usalama ya Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC).

Pongezi hizo zimetolewa na Mwenyekiti wa Machifu mkoa wa Kilimanjaro Frank Marealle, wakati alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari mjini Moshi, muda mfupi mara baada ya kumalizika kwa kikao maalum cha Baraza la Wazee la Ushauri la Kiserikali.

Amesema kitendo cha Rais Samia Suluhu Hassan kuchaguliwa kuwa Mwenyekiti wa SADC, na kufanikiwa kukiongoza kikao hicho cha Kamati ya Siasa, Ulinzi na Usalama ya Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC), alifanikisha kutatua mgogoro wa kisiasa na kiusalama uliokuwepo katika Ufalme wa Lesotho.

  “Kwanza ninampongeza Rais Samia kwa kuweza kufanya maridhiano ya kisiasa hususan katika masuala magumu waliyokuwa yameshindwa kupatiwa muafaka wa utatuzi wa mgogoro wa kiasiasa na kiusalama uliokuwepo katika Uflme wa Lesotho,”amesema.

 Chifu Marealle, amesema Rais Samia amekuwa, Rais wa kwanza mwanamke kuchaguliwa kuwa mwenyekiti wa utatu, ambao unakwenda kulinda masuala ya Siasa, Ulinzi na Usalama  na masuala ya uchaguzi, katika nchi zote za SADC na miongoni mwa mambo ambayo amefanikisha kuyatatua ni pamoja na mgororo wa Lesotho.

“Kwa niaba ya Machifu wa mkoa wa Kilimanjro na Baraza la Wazee la Ushauri la Kiserikali, tunampongeza Rais Samia kuchaguliwa kuwa mwanamke wa kwanza kuongoza nchi za Southern African Development Community (SADC) tunamuombea kwa Mungu ampe maisha marefu ili aweze kuwatumikia Watanzania na nje ya Tanzania.”amesema.

Chifu wa Siha Godfrey Kileo,  amezipongeza nchi zote za Afrika kwa kumchagua kushika wadhifa huo kwani wametambua kwamba anaweza kusimamia shughuli za siasa, ulinzi na usalama, kwetu sisi Tanzania wametupa heshima kubwa.

Awali akizungumza Mwenyekiti wa Baraza la wazee Mkoa wa Kilimanjaro Eliamini Mkongo, amesema Rais Samia amefanya kazi kubwa ya kuwaletea maendeleo Watanzania katika nyamba mbalimbali ikiwemo afya, elimu, maji na miundombinu ya barabara.

Naye Katibu wa Baraza la Wazee Mkoa wa Kilimanjaro Godson Lucas, tunampongeza Rais Samia kwa kuendelea kushughulikia masuala ya migogoro baina ya wakulima na wafugaji, pamoja na kuilinda demokrasia na kusimamia masuala ya ulinzi na usalama kwa nchi yetu.

Kwa upande wake Katibu wa Machifu mkoa wa Kilimanjaro Joseph Mselle, amesema  kwa nafasi aliyopewa ya kuwa mwenyekiti wa SADAC  sehemu inayohusika na mambo ya siasa, ulinzi na usalama, machifu mkoani humo, wameona iko haja ya kumpongeza na kumtia moyo  ili nafasi aliyopewa  aweze kuihudumia vizuri.




Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.