Wananchi mkoani Kilimanjaro, wametakiwa kuweka fedha zao kwa kutumia mifumo ya kibenki ili kuhifadhi fedha zao kwa usalama zaidi na kuacha tabia ya kuhifadhi fedha majumbani.
Meneja Mwandamizi Kitengo cha Biashara kutoka Makao Makuu ya NMB Reynold Tony, ametoa ushauri huo Agosti 26, 2024 wakati wa ufunguzi wa kikao kilichowajumuisha wafanyabiashara ambao ni wate wa NMB, taasisi za umma na wateja ambao sio wateja wa wa benki hiyo kilichofanyika mjini Moshi mkoani humo.
Amesema ni vizuri wafanyabiashara na wananchi wakajenga utamaduni wa kuweka fedha zao katika mifumo ya kibenki hususan kwenye benki ya NMB kwani kwa kutumia mfumo huo wa kibenki, unarahisisha zaidi uendeshaji wa kiuchumi ambao unategemea zaidi matumizi ya utaratibu wa kibenki ambao kwa sasa umerahisisha upatikanaji wake.
Aidha amesema benki ya NMB imeendelea kuongoza katika upatikanaji wa faida baada ya kodi ambapo kwa mwezi wa sita mwaka huu wameweza kupata Sh bilioni 313 na lengo ni kuendelea kushika hiyo namba na kutoa huduma bora kwa wananchi.
Akizungumza kwa niaba ya Meneja wa Kanda ya Kaskazini, Meneja wa Tawi la Nelson Mandela Moshi Roselina Andrew Makulukulu, amesema warsha hiyo ya “Business Club” imewaunganisha wafanyabiashara kutoka wilaya zote za mkoa huo kwa lengo la kuwafahamisha utoaji wa huduma za kibiashra, utoaji wa mikopo, utoaji wa huduma pamoja na kuwapatia taarifa za maboresho mbalimbali ya benki na namna ambavyo NMB imeweza kuyafanya kwa kipindi cha mwaka mmoja.
Amesema kusanyiko hilo la wafanyabiashara (Business Club) wamekuwa wakilifanya kwa zaidi ya miaka mitano sasa tangu kuanzishwa kwake na kwa leo wamewahusisha wafanyabiashara kutoka wilaya zote za mkoa huo.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Chama cha Wateja walioko kwenye mikopo ya ujasiriamali Benki ya NMB mkoa wa Kilimanjaro Valeriani Alphonce Kwayu, amesema tangu kuanzishwa kwa Business Club hiyo, imewawezesha wafanyabiashara hao kuweza kupata mikopo yenye riba nafuu na hivyo kujikwamua kiuchumi.
Nao baadhi ya washiriki wa warsha hiyo Tumaini Kileo na Anandumi Ndossi wamesema bado kuna umuhimu mkubwa wa taasisi za kifedha kuendelea kutoa elimu kwa wananchi juu ya umuhimu wa kuhifadhi pesa benki na kuacha kutunza pesa majumbani.