Viongozi wa Mitaa, Vijiji watakiwa kuendelea kutoa elimu ya uhifadhi wa misitu


Viongozi wa Serikali za Mitaa na Vijiji, vinavyozunguka hifadhi ya msitu wa rau, wametakiwa kuendelea kuwaelimisha wananchi kutunza mazingira na kuacha uchafuzi wa mazingira hasa wa kutupa takataka wanazozizalisha majumbani mwao na kwenda kuzitupa ndani ya hifadhi hiyo.

Kauli hiyo imetolewa jana na Mkuu wa Wilaya ya Mwanga Abdallah Mwaipaya,  kwa niaba ya mkuu wa Wilaya ya Moshi  James Kaji, wakati  wa kuhitimisha Tamasha la Tukacharu Rau Forest  2024 awamu ya pili, lililofanyika ndani ya msitu huo likiwa na lengo la kutangaza utalii wa Msitu wa hifadhi ya Rau.

 

Alisema kuwa hifadhi ya msitu wa rau ni mapafu ya mji wa moshi kwa vile husaidia kufyonza hewa chafu hivyo ni jukumu la kila mmoja kuhakikisha anaendelea kuutunza msitu huo na kuacha mara moja tabia ya watu wanaovamia na kufanya shughuli za kibinadamu.

 

“Mafanikio ya uhifadhi na utalii endelevu yatapatikana endapo serikali, wadau na wananchi wataunganisha nguvu ya pamoja katika kuweka mikakati madhubuti ya kuboresha uhifadhi wa msitu huo wa rau, sanjari na kuendelea kutangaza utalii ikolojia.”alisema.

 

Aidha DC Mwaipaya aliyataka makampuni ya utalii yaliyopo ndani ya wilaya hiyo, pamoja na waongoza utalii, kuwahamasisha watalii kuja kutembelea vivutio vilivyopo ndani ya Msitu wa hifadhi Rau kwani hifadhi hiyo ipo mita tatu kutoka mji wa Moshi.

 

Kwa upande wake Mkuu wa chuo cha Viwanda vya Misitu (FITI) Moshi Dkt. Lupala Zacharia, alisema Misitu inazo fursa nyingi ambazo nyingi hazijaweza kutumika ipasavyo, hivyo kupitia Tamasha la Tukacharu Rau Forest litawezesha kuitangaza vizuri hifadhi hiyo.

Unapotalii msituni unaufanya mti uweze kuhimili, uweze kuongea, lakini pia utaelezwa tabia za miti na faida zake,” alisema Dkt Zacharia.”alisema Dkt. Zacharia.

Dkt, Zacharia ambaye ni mtaalamu wa misiti alisema wananchi wanapofanya utalii wa msituni wanaufanya miti hiyo iweze kuendelea kuishi, iweze kuongea lakipi wataelezwa tabia za miti hiyo na faida zake.

Akisoma taarifa fupi ya Tamasha la Tukacharu Rau Forest  2024 Ofisa Misitu daraja la Pili (TFS) Wilaya ya Moshi Zayana Mrisho Hashim, alisema malengo ya Tamasha hilo ni kuhamasisha utalii ikolojia pamoja na utunzaji wa mazingira na viumbe hai vilivyomo ndani ya hifadhi hiyo.

Aidha alisema tamasha hilo limekuwa na mafanikio makubwa  ambapo kwa mwaka 2023/2024 watalii wameongezeka na kufikia 6,651 ukilinganisha na mwaka 2022/2023 ambapo watalii walikuwa 2034.

Msitu wa hifadhi Rau unazungukwa na Kata tano ambazo ni Njoro, Kaloleni, Msaranga, MjiMpya na Mabogini kwa upande wa Moshi Vijijini.






Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.