Ujenzi wa Veta-Mwanga wamtia hofu Mbunge

MWANGA, KILIMANJARO

Mbunge wa Jimbo la Mwanga Joseph Tadayo, amesema hajaridhishwa na kasi ya ujenzi wa Chuo cha Ufundi Stadi (VETA) kinachojengwa katika Kata ya Kisangiro.

Aidha ameziomba mamlaka zinazohusika na ujenzi huo kuweza kuchukua hatua za makusudi ili kuhakikisha mradi huo unakamilika kwa kiwango kinachotakiwa. 

Tadayo ameyasema hayo Julai 13, 2024, wakati akikagua mradi wa ujenzi wa VETA hiyo na kuona mapungufu yakiwemo ya uchache wa mafundi, waliopo katika eneo la ujenzi wa mradihuo.

"Nimetembelea mradi wa ujenzi wa Chuo hiki cha VETA kinachojengwa hapa Kisangiro, nipende kusema kuwa sijafurahishwa na kasi ya ujenzi wa chuo hiki unavyoendelea, kwenye kazi kubwa kama hii nimekuta kuna mafundi wawili tu, wakati kwenye stoo kuna simenti nyingi na matofali yapo ya kutosha," amesema.

"Mimi si mtaalamu wa masuala ya ujenzi, lakini kuna mapungufu ambayo nimeyaona kwenye mradi huu, ninakwenda kuwasiliana na mamlaka zinazohusika na ujenzi huu ili waweze kuongeza mafundi wa kutosha ili kasi ya ujenzi iweze kufanyika haraka."

Aliongeza kusema kuwa ujenzi wa Chuo hicho ulitakiwa kukamilika Aprili mwaka huu, mkandarasi aliomba kuongezewa muda wa kukamilisha kazi, ambapo alipewa hadi mwezi Julai mwaka huu, lakini bado hataweza kuukabidhi mradi huo.

 Serikali imetenga Sh Bilioni 100 kwa ajili ya ujenzi wa Vyuo vya Ufundi Stadi, huku Wilaya ya Mwanga ikiwa ni miongoni mwa Wilaya 64, ambazo zimebahatika kuwa kwenye mpango huo wa kujengewa Chuo cha Ufundi Stadi.






Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.