Changamoto ya upatikanaji wa Maji Safi na Salama, iliyokuwa ikiwakabili Wananchi wa Wilaya ya Mwanga, imebakia kuwa historia baada ya Serikali ya Awamu ya Sita, kutekeleza mradi mkubwa wa Maji wa Same-Mwanga-Korogwe wenye zaidi ya Sh bilioni 300.
Wakizungumza na 'Kisena Update' Wananchi hao wamesema, wamefurahia mno kutekelezwa kwa mradi huo wa maji ambao licha ya kuwatua ndoo kichwani akina mama, pia utawaepushia magonjwa ya mlipuko yaliyokuwa yakiwapata kutokana na kutumia maji yasiyo safi na salama.
Akizungumza kwa niaba ya wenzake Mkazi wa Mwanga Seleman Kisaka, amesema changamoto ya maji ilisababisha wananchi wengi kushindwa kufanya shughuli zao za kiuchumi kutokana na kutumia muda mwingi wakihangaika kutafuta huduma ya maji.
Naye mkazi wa Mwanga Hinja Solomon Msuya amesema, maji ambayo walikuwa wakiyatumia yalikuwa sio salama kiafya kwao, kutokana na maji hayo kuwa na magadi.
Amesema kuwa uwepo wa mradi huo wa maji, utawapa muda wa kutosha wananchi kufanya shughuli za maendeleo kwa kuwa awali, walikuwa wakitumia muda mrefu kutafuta maji.
"Kwa kipindi cha miaka 19 kilio cha Wananchi wa Wilaya ya Mwanga ilikuwa ni maji, tangu aliyewahi kuwa Mbunge wa Jimbo la Mwanga Profesa Jumanne Maghembe akiwa Waziri wa Maji,"amesema.
Akizungumza na Wananchi wa Mwanga, Mbunge wa Jimbo hilo, Joseph Tadayo, amesema mradi wa maji ulikuwa ndio mtihani wake wa kwanza wakati anaingia katika nafasi ya kuwatumikia wananchi.
"Jimbo la Mwanga lina Kata 20, Vijiji 72 na Vitongoji 282, tambarare ya Magharibi, imekuwa na changamoto kubwa ya maji kwa miaka yote tangu Wilaya ya Mwangu kuanzishwa na mradi huu wa maji Same-Mwanga-Korogwe ndio ulikuwa mtihani kwangu, naishukuru Serikali imeniondoa kwenye mtego huo,"amesema Mbunge Tadayo.
Aidha Mbunge Tadayo, amewahimiza Wananchi kupeleka maombi yao kwa wingi ili waweze kuunganishiwa maji moja kwa moja majumbani mwao.
Katika hatua nyingine Mbunge Tadayo amemshukuru Rais Samia kwa nia yake ya dhati ya kuhakikisha mradi huu wa maji unakamilika ambapo kwa sasa wananchi wameanza kupata maji hayo.
Serikali kwa kushirikiana na Benki ya Maendeleo ya Kiarabu (BADEA), Mfuko wa Maendeleo wa Nchi zinazozalisha Mafuta (OFID) na Kuwait Fund, imetekeleza mradi wa maji Same-Mwanga-Korogwe, ambao umelenga kusambaza maji katika Miji ya Same na Mwanga pamoja na Vijijini 38 kwenye Wilaya za Same na Mwanga na Vijiji vitano katika Wilaya ya Korogwe.




