Mwanga wapeleka kilio uvamizi wa Tembo mashambani

KIVISINI, MWANGA

Wananchi wilayani Mwanga mkoani Kilimanjaro wameeleza masikitiko yao kutokana na changamoto ya muda mrefu ya wanyamapori aina ya tembo ambao wamekuwa wakiharibu mazao yao na kutishia usalama wao. 

Vijiji vya Butu, Toloha, Kwakoa na Kigonigoni hutikiswa zaidi na tembo na kusababisha ukosefu wa amani na mazao kuharibiwa.

Wakizungumza mbele ya mbunge wa Jimbo la Mwanga Joseph Tadayo alipozuru katika mbalimbali kwenye jimbo lake ikiwamo kata ya Kivisini wamesema tembo wamekuwa wakiingia kwa wingi kipindi cha kilimo wakitokea Hifadhi ya Mkomazi (Tanzania) na Tsavo (Kenya). 

Wananchi hao wameongeza kuwa juhudi za lazima zitakiwa kufanyika ikiwamo ya kupeleka askari wanyamapori kuwaondoa na kujenga mabanda ya ulinzi ili tembo hao wasikaribie mashamba yao. 

“Kwenye kijiji chetu cha Msangeni, tembo wamegeuza uwanja wa kufanya mazoezi, Tunaiomba Serikali tujengewe mabanda ya ulinzi maeneo yote yenye tatizo la tembo, na kupelekewa askari wa wanyamapori ili waweze kuwaondoa pia watuletee vifaa vya vipulizi pamoja na kujenga kituo cha kuwafukuza wanyama hawa ili wananchi wapate unafuu wa kuyalinda mazao yao.", amesema mkazi wa kijiji cha Msangeni Emmanuel Justin. 

Kwa uchungu mwingi mkazi wa kijiji cha aliyejitambulisha kwa jina moja tu la Mustafa alisimulia namna alivyonusurika kuuawa na tembo waliofika hadi nyumbani kwake na kuanza kupiga mayowe ambapo wananchi walikuja na tochi na kuanza kuwafukuza. 

"Changamoto ya tembo imezidi katika maeneo yetu hawataki wanapomaliza kula mazao kuna uwanja huja na kukaa hapo, kwenye shamba langu hakuna nilichoweza kuvuna maana wamekula mahindi yote," amesema Mustafa 

Akizungumza na Kisena, Diwani wa kata hiyo Mwalimu Ziada Mziray amesema katika vijiji mbalimbali katika kata ya Kivisini kikiwamo kijiji cha Msangeni ambacho diwani huyo huishi huko, tembo wamekuwa kero kubwa. 

"Changamoto ya wanyamapori waharibifu , tembo asilimia 80 ya wakullima katika kata ya Kivisini wamepoteza nguvu kazi yao kwani mazao yote yameliwa na tembo," alisema Mziray. 

Tembo hao wamekuwa wakikusanyika hapo kwa ajili ya kupumzika na pindi msimu wa kiangazi unapoanza huondoka eneo hilo.

 









 

 


Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.