MWERO, MWANGA
MBUNGE wa Jimbo la Mwanga, Mkoani Kilimanjaro Joseph Tadayo, ametoa rai kwa uongozi wa TASAF Wilayani humo kuongeza kasi ya ujenzi wa madarasa shule ya Msingi ya Mwero, ili wanafunzi waanze kuyatumia.
Tadayo ametoa rai hiyo Julai 8, 2024, Wakati akiwa katika ziara ya kukagua utekelezaji wa shughuli za Maendeleo Wilayani humo, ikiwemo utekelezaji wa mradi wa shule hiyo iliyoko Kata ya Kirongwe.
Amesema serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt Samia Suluhu Hassan imetoa fedha nyingi kwa ajili ya kuboresha elimu na kwamba ni vyema miradi hiyo ikatekelezwa kwa haraka ili wananchi wanufaike.
“Katika kutekeleza swala hilo, Serikali pia imetoa fedha kwa ajili ya kuboresha miundombinu ya shule kongwe ikiwemo hii ya Mwero, ni vyema mamlaka huska ndani ya TASAF zikafanyika haraka kumalizia mradi huu ili wanafunzi waanze kuyatumia madarasa haya”, alisema.
Akiongea wakati wa ziara hiyo, Afisa Elimu (Msingi) Wilaya ya Mwanga Jeremiah Malyo, alisema kuwa Shule ya Msingi Mwero ni miongoni mwa shule kongwe nchini ambayo imetoa viongozi wengi.
“Pamoja na umaarufu unaotokana na historia yake ya miaka mingi, shule hii ilikuwa na miundombinu chakavu sana; tunaishuru Serikali kwa kutuletea mradi wa TASAF ambao umetoa kiasi cha Sh milioni 178.3 ambazo zinatekeleza ujenzi wa madarasa mawili, ofisi na nyumba za walimu”, alisema.
Aidha amemshukuru Rais Samia kwa kuleta fedha za BOOST ambazo zimewezesha kukarabati shule kongwe zikiwemo zile zilizoko Wilayani Mwanga, ambazo nyingi kati ya hizo zilikuwa na miundombinu chaavu sana.
Aidha alisema pia Serikali imetoa jumla ya Sh milioni 100 kwa ajili ya shule ya Msingi Kifula na Sh milioni 348 kwa ajili ya shule msingi Ndolwe.
"Ktika mwaka wa fedha 2024/2025 Serikali imeipatia halmashauri ya Mwanga kiasi cha Sh milioni 348 kwa ajili ya kujenga shule mpya ya msingi Mlevo."
Naye Mratibu wa TASAF Wiaya ya Mwanga George Mfinanga, alisema kuwa mradi wa shule ya msingi Mwero uliletewa fedha kiasi cha Sh milioni 178.3 kwa ajili ya ujenzi madarasa 2, Ofisi ya mwalimu, nyumba ya walimu na choo cha wanafunzi chenye matundu sita.
“Mradi huu ulianza kutekelezwa Januari mwaka huu na ulitazamiwa kukamilika mwezi Juni 2024; kwa sasa madarasa mawili na ofisi ya mwalimu yako kwenye hatua ya upauaji, hii inatokana na changamoto ya mvua nyingi kunyesha zaidi jambo lililopelekea mrdai kusimama kwa muda”, alisema.
Nao baadhi ya wananchi wa eneo hilo wameipongeza serikali kwa kutoa fedha kwa ajili ya ukarabati na ujenzi wa madarasa mapya jambo ambalo wamesema litasaidia kutoa mazingira mazuri kwa wanafunzi kuendelea na masomo yao.
“Majengo ya shule hizi yalikuwai mabovu, yenye nyufa kubwa zinazoweza kuhatarisha maisha ya watoto, wanafunzi walitaajiwa kuwa baada ya kutoka likizo ya mwezi wa saba wangeingia katika madarasa mapya lakini hadi sasa majengo hayo hayajakamilika, alisema mmoja wa wakazi hao Shaban Mmbaga.
Naye mkazi mwingine Twalibu Abdalla, alisema inasikitisha kuona ya kuwa mradi wa ujenzi wa shule hiyo, unasuasua huku baadhi ya madawati yaliyotengenezwa yakiwa yamepinda kabla hata hayajaanza kugtumika.





