
Mwenyekiti wa CCM wilaya ya Moshi, Faraj Swai akizungumza na Kisena Update Blog kuhusu namna chama hicho kinavyoweza kushinda uchaguzi ujao wa serikali za mitaa baadaye mwaka huu. (Picha na KISENA).
MOSHI, KILIMANJARO
MWENYEKITI wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Moshi Mjini, mkoani Kilimanjaro, Faraj Swai, amesema kuwa njia pekee ya chama hicho tawala kuendelea kushinda chaguzi mbalimbali ni kutekeleza kwa umakini Ilani ya chama hicho.
Swai aliyasema hayo jana kwa nyakati tofauti wakati akiwa katika ziara ya kukagua utekelezaji wa Ilani ya uchaguzi ya CCM ya mwaka 2020/2025 katika wilaya hiyo.
“Wakati tukiomba ridhaa ya wananchi ya kushika dola, tuliwasilisha ilani yetu yenye malengo ya kuleta maendeleo, hivyo utekelezaji wake ndiyo tiketi ya kuipa ushindi CCM kwenye uchaguzi wa serilali za mitaa mwaka huu na uchaguzi mkuu wa mwakani”, alisema.
Akizungumza jana na Wajumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Kata ya Soweto Manispaa ya Moshi, Swai, aliwataka viongozi hao kuhakikisha kwamba wanawahamsisha wananchi kujiandikisha kwenye daftari la kudumu la wapiga kura kwa wale ambao ndiyo wanajiandilisha upya ili kuongeza idadi ya wana CCM ambao watakipa chama hicho ushindi kwenye chaguzi mbalimbali.
“Pia hakikisheni mnawahamasisha wale ambao walikuwa washajiandikisha ya kuwa wanakwenda kuhakiki taarifa zao katika daftari hilo katika maeneo waliyojiandikishia”, alisema.
Awali Katibu wa CCM Wilaya ya Moshi Mjini Frida Kaaya, alitoa rai kwa viongozi hao kuhakikisha wanajitayarisha kwa ajili ya daftari la CCM la makazi kwa ajili ya uchaguzi wa Serikali za Mitaa, unaotarajia kufanyika baadaye mwaka huu.
“Wanachama hai wote wa CCM wahakikishe wana kwenda kujiandilisha kwenye daftari la chama kwani ndiyo itakuwa tiketi ya mwanachama kushiriki uchaguzi wa ndani wa CCM wa kuteuwa wawakilishi wa CCM kwenye uchaguzi wa Serikali za Mitaa”, alisema.
Akifafanua zaidi Kaaya, alisema watakaopiga kura za maoni kwa ajili ya kuteua wawakilishi wa CCM kwenye chaguzi za wenyeviti wa Serikali za Mitaa ni wana CCM walio na kadi za CCM.
“Mwanachama atahitajika kuonyesha kadi yake ya CCM ndipo aruhusiwe kupiga kura ya maoni ya kuteua mgombea atakaeipeperusha bendera ya CCM kwenye chaguzi za Serikali ya Mitaa”, alisema.
Kwa upande wake Katibu Mwenezi wa CCM Wilaya ya Moshi Mjini Athuman Mfuchu, alitoa rai kwa wana CCM kuteua wagombea ambao wanakubalika kwa wananchi.



