![]() |
Mkuu wa Takukuru mkoa wa Kilimanjaro Mussa Chaulo |
Taasisi ya kuzuia na kupambana rushwa TAKUKURU mkoa wa Kilimanjaro, imesema wamejipanga kikamilifu kuelekea uchaguzi wa Serikali za Mitaa utakaofanyika mwaka huu.
Kamanda wa TAKUKURU Mkoa wa Kilimanjaro Mussa Chaulo, ameyasema hayo Julai 26,2024 wakati akizungumza na Waandishi wa habari Ofisini Kwake, wakati akitoa taarifa ya utekelezaji wa majukumu Takukuru kwa kipindi cha robo ya Nne ya Mwaka 2023/2024 kuanzia Aprili hadi Juni mwaka 2024.
Amesema taasisi hiyo, imejipanga kutoa elimu na kuzuia rushwa kwa Wananchi na wagombea ili kuhakikisha uchaguzi wa Serikali za Mitaa unakuwa huru na haki kwa mwaka huu na Uchaguzi mkuu wa mwaka 2025.
Chaulo, amesema wako baadhi ya wagombea hutoa takrima kwa wananchi kitu ambacho hakitofautia na rushwa, hivyo katika kipindi chote cha maandalizi ya uchaguzi wa Serikali za Mitaa na uchaguzi mkuu hakitaruhusiwa.
Aidha Chaulo, amewatoa hofu wanachi wasiogope kutoa taarifa kwani kuna sheria inayowalinda watoa tarifa pindi watakapo toa taarifa za rushwa katika ofisi za Takukuru.
Akizungumzia tathmini ya kazi kwa mwaka 2023/2024 na mikakati ya mwaka 2024/2025 Chaulo, amesema kuwa kwa mwaka wa fedha 2024/2025 Takukuru Mkoa wa Kilimanjaro imeendelea kuwashirikisha wadau mbalimbali katika mapambano dhidi ya rushwa na kuweka kipaumbele katika kuzia vitendo vya rushwa visitiokee kwenye miradi mbalimbali ya maendeleo ambayo inaendelea kutekelezwa ndani ya mkoa huo.
Nao baadhi ya wakazi wa Manispaa ya Moshi Daniel Michael na Miryam Mushi, wamesema elimu zaidi inatakiwa kutolewa kwa jamii kuhusiana na masula ya rushwa kuelekea katika uchaguzi wa serikali za mitaa.
“Watu wengi wamekuwa wakikosa haki zao za msingi katika maeneo mbalimbali kwa sababu ya rushwa, tunaiomba Takukuru kuendelea kuangaza katika nyanja mbalimbali ili kuweza kudhibi suala la rushwa kwenye uchaguzi.”amesema Michael.
Naye Mkazi wa Njoro Gadson Mdee, amesema elimu zaidi ya masuala ya rushwa iendelee kutolewa kwa wananchi, ili kutokukubali kupewa takrima au zawadi kutoka kwa watia nia ili kuwashawishi wananchi waweze kuwachagua watu ambao wameanza kuonesha nia za kutaka kugombea nafasi mbalimbali za uongozi.
Mkazi mwingine wa Kata ya Pasua Gasper Shirima, amesema wananchi wasikubali kurubuniwa kwa rushwa ya Sh 5,000 au Sh 10,000 ili waweze kuwachagua viongozi, bali kuangalia mtu ambae anakubalika kwenye jamii na kuepeuka kuchagua watu ambao wanataka kupata nafasi hizo kwa njia ya rushwa.